Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WADAU wa michezo wamemwomba Mratibu wa Kombe la Muungano Mufindi,
Daud Yassin, kufikiria zaidi uamuzi wake wa kustaafu kuandaa mashindano
hayo na kuongeza muda zaidi wa kuratibu kwa lengo ya kuyaokoa yasife.
Kati ya waliomuomba Yassin kubatilisha uamuzi wake, ni Mkurugenzi wa
Idara ya Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo, ambaye alikuwa mgeni
rasmi katika fainali ya kombe hilo iliyopigwa mwishoni mwa wiki kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Igowole, Mufindi mkoani Iringa na kushuhudiwa
timu ya Benki ya Wananchi Mufindi (Mucoba), ikiibuka bingwa mpya baada
ya kuwavua Mbaspo ya Mbeya.
Thadeo, alimtaka mratibu huyo kuongeza muda zaidi wa kuratibu
mashindano hayo, huku akimwandaa mtu mwingine aweze kuyaendeleza.
Alisema ni uamuzi wa busara wa Yassin kung’atuka, lakini kabla ya
kuachia madaraka hayo, hana budi kutengeneza mazingira kwa mtu ambaye
atakuja kushika nafasi hiyo ili aweze kuendeleza mazuri ya Kombe la
Muungano.
“Usiondoke ghafla ndugu yangu, kwanza weka mazingira safi kwa
kumwandaa mtu ambaye ataweza kuyasimamia na shirikiana na wadau wa
michezo wilayani hapa na kisha unaweza kufanya maamuzi yako ya
kung’atuka,” alisema Thadeo.
Aliwataka waratibu wa mashindano hayo kupanua wigo kwa kushirikisha
michezo mingine itakayohusisha jamii husika, kwa kuanzia ngazi ya
kijiji hadi tarafa na kisha mikoa.
Thadeo, aliwashukuru wadau wote waliofanikisha mashindano ya Muungano
kufana na waliyoyaunga mkono na kuwataka wafadhili zaidi kujitokeza
katika kuyapa sapoti miaka inayokuja.
Mdau mwingine wa michezo, Alex Kalinga, alisema kuwa kustaafu kwa
Yassin kuratibu mashindano ya Kombe la Muungano ni mshituko mkubwa
katika tasnia ya michezo na kumtaka kuongeza miaka zaidi, kwa lengo la
kumwandaa mtu mwingine aweze kuyasimamia kwa uadilifu na kuendeleza
vipaji vya vijana.
Alisema mashindano ya Kombe la Muungano Mufindi, yameweza kuvumbua
vipaji vingi katika Wilaya ya Mufindi na mikoa ya jirani, hivyo hofu
kubwa ni kusimama kwa mashindano hayo na kufa kabisa kama Yassin
ataamua kustaafu.
Alisema upeo mkubwa wa mratibu huyo ndiyo chachu ya mashindano hayo kuwa makubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania.
“Itachukua muda sana kumpata mtu atakayevaa viatu vyake kwa sasa,
hivyo ni jukumu la wadau kukaa na Yassin kuweza kujadili jinsi gani
atamwachia mtu na ikiwezena aahirishe kustaafu kuandaa mashindano
haya,” alisema Kalinga.
Mwalimu Wilson Ngongi, alisema Yassin ataacha mzigo mzito kwa jamii
ya wanamichezo akiamua kweli kustaafu kuratibu mashindano hayo, ambayo
yamejizolea mashabiki na kuvumbua vipaji kwa miaka zaidi ya 18.
Alisema Watanzania wengi ni watu wa kukwepa majukumu ambayo hayana
maslahi, lakini kwa Yassin ameweza kuandaa mashindano hayo kwa fedha
zake za mfukoni hadi yakawa makubwa na kushirikisha mikoa mingine
ikiwemo Zanzibar.
“Naomba sana Yassin atusaidie kuendelea kukuza vipaji vya vijana,
kwani hili hakuna mtu mwingine kwa sasa atakayeweza kuyaendeleza na
mwisho wa siku mashindano haya yatakufa,” alisema Ngongi.
Kwa upande wake, Yassin alisema ameanza kuandaa mashindano ya Kombe
la Muungano Mufindi akiwa kijana mdogo, lakini kwa sasa umefika wakati
wa kustaafu na kuwaachia wengine kuyaendeleza.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment