Home » » USAJILI WA WAKULIMA KIDIJITALI WAFIKIA ASILIMIA 64.7

USAJILI WA WAKULIMA KIDIJITALI WAFIKIA ASILIMIA 64.7

Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga.  Usajili wa wakulima kidijitali katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga umefikia asilimia 64.7, taarifa kutoka Idara ya Kilimo ya  Halmashauri hiyo inaonesha.

Taarifa kutoka idara hiyo inaonesha kuwa tangu zoezi la usajili lianze katika msimu wa kilimo wa 2022/23, tayari wakulima 23,222 kati ya 35,876 wamejisajili katika mfumo huo wa kidijitali.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Dkt. Kung’e Nyamuryekung’e Ijumaa ya Julai 26 alisema kuwa kwa kujisajili kidijitali, wakulima wataweza kupata huduma mbalimbali kiurahisi.

Alisema miongoni mwa huduma ambazo wakulima watapata kupitia kanzidata ya usajili ni mbolea za ruzuku, ugani na taarifa za masoko.

Sanjari na faida hizo, usajili wa wakulima kwenye mfumo, utaiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.

“Kwa kujisajili katika mfumo wa kidijitali mtaweza kununua mbolea kwa bei nafuu, mtaongeza uzalishaji na kuboresha maisha yenu na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,” alisema Dkt. Nyamuryekung’e.

Sekta ya kilimo ambayo ndio muhimili wa uchumi wa Tanzania, kwa mujibu wa taarifa kutoka wazara ya Kilimo, mwaka jana iliajiri asilimia 65.6 ya nguvu kazi ya Taifa na kuchangia asilimia 26.5 kwenye pato la Taifa.

Ni katika muktadha huo, Dkt. Nyamuryekung’e aliwasihi wakulima wa Mji Mbinga ambao bado hawajajisajili kwenye mfumo wa kidijitali, wafanye hivyo ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na Serikali na hivyo kuongeza mchango wao kwenye uchumi wa nchi.

Alisema zoezi la usajili, ambalo ni bure, linafanywa na maafisa kilimo wa vijiji au kata.

Taarifa zinazohitajika, alieleza, ni kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, mahali shamba lilipo, aina ya mazao yanayo limwa na ukubwa wa shamba.

Katika mazingira ambayo kilimo ndio sekta kuu ya uchumi, maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, yanategemea zaidi ufanisi katika sekta hiyo.

Na ndio maana serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira ya dhati ya kufanya mapinduzi katika sekta hiyo.

Hii inadhihirishwa na kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh294.16 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh1.25 tirioni mwaka huu wa fedha.

Sehemu ya bajeti ya wizara inatumika kutoa ruzuku kwa wakulima ili waweze kununua mbolea kwa bei nafuu.

Hatua hii ni muhimu katika kuwezesha uzalishaji wenye tija na hivyo kuwa chachu ya kuongeza kipato kwa mkulima mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa