Home » » MRADI WA SLR WATENGA EKARI 28,000 UREJESHAJI UOTO WA ASILI

MRADI WA SLR WATENGA EKARI 28,000 UREJESHAJI UOTO WA ASILI

Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) imetenga ekari 28,000 za misitu ya jamii iliyopo katika vijiji vya Halmashauri saba (07) kwa ajili ya urejeshaji wa uoto wa asili.

Hayo yamebainishwa Julai 31, 2024 Mkoani Iringa na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa mahojiano na waandishi wa vyombo vya habari katika kikao cha siku moja cha kamati ya kitaifa ya usimamizi wa mradi kilichopokea taarifa ya mradi huo.

Dkt. Mapunda amesema tangu kuanza kwa mradi mwaka 2021, wataalamu walibainisha baadhi ya maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri zinazotekeleza mradi ili kuonesha juhudi na hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika urejeshaji wa uoto wa asili.

“Moja ya eneo ambalo tunaweza kujivunia kwa sasa katika mradi ni urejeshaji wa uoto wa asili…kati ya vijiji 54 vya mradi tuna vijiji ambavyo kwa sasa suala la uoto wa asili limeleta manufaa manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Mapunda.

Ameongeza kuwa kupitia mpango wa urejeshaji, baadhi ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji, huduma za mifumo ikolojia pamoja na shughuli za kilimo mseto.

Aidha Dkt. Mapunda amesema kupitia uhifadhi misitu jamii, mradi umewezesha shughuli endelevu na wezeshi ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa na kusaidia uhifadhi wa mazingira na kufanya usimamizi wa rasilimali zilizopo na kuandaa mpango matumizi bora ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kidunia ya kurejesha ekari Milioni 2.5 za uoto wa asili nchini ifikapo mwaka 2030.

Kuhusu vipaumbele vya bajeti ya mradi kwa mwaka 2024, Dkt. Mapunda amesema jumla ya vipaumbele vitano vimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mradi ambapo moja ya kipuambele hicho ni usimamizi wa biashara ya kaboni.

Ametaja vipaumbele vingine ni kuwezesha wakulima kutekeleza shughuli za miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ufugaji endelevu, kuhamasisha shughuli mbadala za kiuchumi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya shughuli za uzalishaji mali.

Kwa upande wake Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Doyi Mazenzele amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuweka mikakati ya pamoja kwa kuendelea kuhimiza jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa bioanuai ambazo zinachangia upatikanaji wa huduma ikolojia.

“Tumeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wananchi na wasimamizi wa miradi katika maeneo ya halmashaur” amesema Mazenzele.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Robert Masunya amesema Halmashauri hiyo imeendelea na juhudi mbalimbali za uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili kwa kuhimiza shughuli wezeshi zisizoharibu mazingira ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tumeendelea kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinapewa kipaumbele katika maeneo yote ndani ya Halmashauri ambayo yanatekeleza mradi kwa ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuhamasisha wananchi kutunza maeneo hayo" amesema Masunya.

Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unatarajia kukamilika mwaka 2025 na kunufaisha jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54. Halmashauri zinazonufaika na mradi ni Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.


 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa