Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
FAINALI za 18 za mashindano ya Kombe la Muungano Mufindi
zilimalizika juzi kwa Benki ya Wananchi Mufindi (Mucoba Fc), kunyakua
taji kwa kuwafunga mabingwa watetezi Mbaspo Academy ya jijini Mbeya kwa
changamoto ya penalti 7-5 katika mchezo mkali uliofanyika uwanja wa
shule ya Msingi Igowole, Mafinga.
Katika mchezo huo ambao Mgeni Rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo, hadi dakika 45 zinakamilika
kuashiria mapumziko, hakuna nyavu iliyokuwa imetikiswa.
Kipindi cha pili, kilianza kwa timu zote kusomana, lakini walikuwa ni
Mucoba walioanza kujipatia bao dakika ya 70 likifungwa na David Mhanga
kabla ya kuongeza la pili dakika ya 75.
Mbaspo walikuja juu na kupata bao dakika ya 84 likifungwa na Soud
Mlindwa kabla ya Thabit Juma kuchomoa dakika ya 90, ndipo changamoto ya
mikwaju ya penalti alipochukua nafasi.
Penalti za Mbaspo zilifungwa na Eliah Jimmy, Mpoki Mwansansu, Masoud
Yusuph, Soud Mlindwa na Boaz Patson huku Thabit Juma na Michael Masinga
wakikosa.
Mucoba waliofunga ni Benjamin Mlowe, Ima Mwakajinga, Stanley
Mwazangila, Elisha Mwasieni, Denis Lameck na Daud Mwanga huku aliyekosa
ni Reward Abraham. Katika mikwaju hiyo, shujaa aliibuka Kipa wa Mucoba
aliyepangua penalti mbili.
Bingwa wa mashindano hayo, Mucoba ilijinyakulia sh milioni 3, Kombe
lenye thamani ya sh milioni 1.2 na medali za dhahabu, mshindi wa pili
Mbaspo, iliondoka na kitita cha sh milioni 1.5, waamuzi bora Steven
Makuka, Hashim Mgimba na Erasto Msalilwa waliojipatia sh 50,000 kila
mmoja, mchezaji bora aliibuka Hussein Juma Igowole Sekondari aliyepata
sh 200,000 mfungaji bora Shadrack Tamimu wa Mbeya City sh 200,000 na
timu yenye nidhamu ikaibuka Mbeya City iliyojipatia sh 500,000 na
kombe.
Kombe la Muungano Mufindi 2014 linaratibiwa na Daud Yassin na kudhaminiwa na Chai Bora, Asas Limited, Mucoba na PPF.
chanzo :Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment