Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
TAASISI
za kifedha zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali
nchini, zimetakiwa kuacha mfumo wa kuwakandamiza wanachama wake kwa riba
kubwa, kwa madai kuwa zinachangia kudumaza shughuli za kiuchumi na
mustakabali wa maisha ya wateja wake.
Rai hiyo ilitolewa mjini hapa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
Mfuko wa Mama Bahati Foundation (MBF), Japhet Makau, katika mafunzo ya
wanachama viongozi wa vikundi vya asasi hiyo.
Alisema taasisi za kifedha zisitegemee zaidi kujiendesha kwa riba za
wanachama, kwani hatua hiyo itawafanya wateja kufilisika kwa kushindwa
kurejesha mikopo, na kuishia kufilisiwa mali zao na kurejea katika hali
ya umasikini.
“Wito wangu kwa asasi za kifedha wanapofanya shughuli zao na wateja
wao hao wadogo wadogo lengo kuu linapaswa liwe ni kuwasaidia masikini
kwa kuwatoa katika hali duni na kuwawezesha kuwa katika hali nzuri,
tusiweke suala la faida mbele, kwani ukiweka lengo la faida utamdidimiza
masikini na kuwa masikini zaidi,” alisema Makau.
Alisema mfuko huo hadi sasa umeshatoa zaidi ya sh bilioni 5 kwa
wanawake wa Manispaa ya Iringa, Iringa Vijijini na Wilaya ya Kilolo na
kusema kuwa lengo la mfuko huo si kutengeneza faida bali ni kuwawezesha
wafanyabiashara wenye mitaji midogo.
Mwanzilishi wa mfuko huo, Askofu Mkuu mstaafu, Donald Mtetemela,
alisema upo umuhimu wa kuendeleza mpango huo kwa kinamama, ili kuwainua
kiuchumi, baada ya mama aliyemsaidia sh 10,000 kuendeleza biashara yake
kuonyesha uaminifu, hatua iliyofanya kumuongeza kiwango hadi kufikia sh
50,000.
Hata hivyo, mama huyo, Diana Mbembela aliyekuwa akitembeza ndizi mitaani, hivi sasa ni marehemu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment