MKUU wa Wilaya
ya Kilolo mkoani Iringa Gerald Guninita amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi
wa shule kutowaruhusu watoto wao kufanya biashara zenye mazingira hatarishi,
ili kuwaepusha na changamoto zinazowakwamisha wanafunzi kutomaliza masomo.
Guninita ameyasema hayo wakati akipokea msaada
wa Bweni la Wasichana wa shule ya sekondari ya Lundamatwe,jengo liligharimu
zaidi ya shilingi Milioni 76.8, msaada uliotolewa na kampuni ya Newforest
inayojishughulisha na upandaji wa miti mkoani Iringa.
Aidha Guninita amesema baadhi ya wanafunzi
wamekuwa wakiingia katika vishawishi kwa kutumiwa na wazazi/ walezi kufanya
biashara zisizostahili ikiwa pamoja na uuzaji wa pombe katika vilabu, jambo
linalosababisha hasa mabinti kuingia katika ngono na kupata mimba.
Amesema jamii inapaswa kuwalinda wanafunzi hasa
mabinti ikiwa pamoja na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanakaa katika mabweni,
ili waweze kupata muda mwingi wa kujisomea, kutokana na ukweli kuwa wanafunzi
wamekuwa wakipatiwa majukumu mengi wawapo nyumbani.
Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuchangia mifuko 50
ya Saruji katika shule hiyo ili kuwaunga mkono juu ya ujenzi wa bweni lingine
la wavulana, huku akiwahimiza wananchi kuchangia sekta ya elimu kwa kuwekeza
zaidi kwa wanafunzi ambao ni viongozi wa siku zijazo.
Hata hivyo mkurugenzi mkuu wa Newforest Bw. Rob
Newborn amesema atahakikisha kampuni yake inashirikiana vyema na jamiii
inayouzunguka mradi kwa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ili kuleta
tija ya uwepo wa kampuni yake.
0 comments:
Post a Comment