Meneja wa kiwanda cha Pareto Martin Oweka kilichoko Wilayani Mufundi katika mji wa Mafinga.
======== ====== ========
KIWANDA CHA PARETO(PCT) WAPATA HASARA BILIONI 1.4
Na Denis
Mlowe,Mufindi
KIWANDA cha Pareto(PCT) cha Wilayani Mufindi, mkoani
Iringa kimepata hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.4 baada ya kushindwa
kununua pareto kwa wakulima na kuizalisha kwa kipindi cha miezi miwili. Meneja
wa kiwanda Martine Oweka alisema mpaka sasa mitambo ya kuzalishia zao hilo
ilisimama kwa muda kutokana na kukosekana kwa malighafi hiyo baada ya kuwepo
kwa wanunuzi wengi, ambao wamekuwa wakisafirisha nje ya nchi licha ya kuwepo
kiwanda.
Alisema hasara kubwa
inatokana na uwekezaji wao katika zao hilo ambapo, kwenye msimu wa kilimo
walitumia Sh milioni 500, kuwanunulia wakulima miche ya pareto, elimu juu ya
kilimo hicho sambamba na ujenzi wa maeneo ya kukaushia zao hilo, ili kuongeza
sumu. " Mwezi Julai ilikuwa tupate tani 100 za pareto kwa wakulima lakini
tuliambulia tani 20 wakati mwezi huu wa agosti kati ya tani 200 ambazo ilikuwa
tukusanye, tumeambulia tani 30 tu, hii ni hasara kubwa sana kwetu hatukuwa na
kibali cha kununua pareto kwa wakulima japo hiki ni kiwanda pekee
Tanzania,”alisema Oweka.
Alisema kibali cha
kununua zao hilo kwa wakulima ilikuwa wapatiwe mwezi juni mwishoni, lakini
badala yake walipewa August 21, mwaka huu kikiwa kimechelewa kwa miezi miwili.Hata
hivyo alisema hasara ya Sh Bilioni 1.4 waliyoipata kwa kushindwa kuzalisha zao
hilo, inawaghalimu wakulima ambao, wengi wao wamehifadhi pareto ndani kinyume
cha taratibu za zao hilo, ambalo ubora wake hutegemea ukali wa sumu.
“Mkulima akivuna
Pareto halafu akahifadhi ndani kwenye unyevu kwa muda mrefu inapoteza sumu
kiasi ambacho hata sisi wanunuzi inakuwa vigumu kuinunua kwani, ubora wa pareto
ni kiwango cha sumu iliyopo,”alisema.Aliongeza kuwa kushindwa kununua pareto
hiyo kumeisababishia hasara serikali kwa kuwa imekosa fedha za kigeni ambazo
hutokana na mauzo ya nje ya zao hilo mara baada kuzalishwa kiwandani hapo. Aliwataka
wakulima kutokata tamaa na badala yake waendelee kuzalisha zao hilo na kuiomba
serikali kulinda soko la pareto.
Kwa upande wao
wakulima, wameiomba serikali kuhakikisha kuwa zao hilo halifi na kuona namna ya
kulinda viwanda vya ndani vyenye uhakika wa soko badala ya kuruhusu soko huria,
wakati malighafi hiyo hata ndani ya nchi haitoshelezi mahitaji. Uwezo wa
kiwanda cha Pareto cha Mafinga ni kuzalisha tani 6,000 kwa mwaka lakini badala
yake, kimekuwa kikiambulia tani 2,5000 pekee.
0 comments:
Post a Comment