Jeshi la Polisi mkoani hapa lilimshikilia na kumuachia kwa dhamana
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa tuhuma za kuratibu
matukio mawili ya kihalifu likiwamo la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi
Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM Iringa Mjini, Alfonce Muyinga.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Julisu Mjengi amesema mbunge huyo alikuwa
akitafutwa kwa muda akituhumiwa kuratibu utekelezwaji wa matukio mawili
ya kihalifu likiwamo la Januari 17 la kuchomwa kwa nyumba aliyokuwa
akiishi Muyinga.
Mjengi alitaja tukio la pili kuwa ni lile la Januari 15 la kubomolewa
kwa nyumba ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwangata Chadema, Anjelus
Mbogo aliyejizulu nafasi yake na kuhamia CCM.
"Mchungaji Msigwa tulikuwa tukimtafuta kutokana na kuhusika kwake katika
kuratibu matukio mawili ya kihalifu, lile la Januari 15 la kubomoa
nyumba ya aliyekuwa diwani aliyehama Chadema na kujiunga na CCM pamoja
na tukio la kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa Jumuiya ya Vijana
wa CCM Alfonce," amesema Mjengi na kuongeza;
"Na jana (Jumatatu) amejisalimisha mwenyewe hivyo tumemhoji hadi majira
ya saa tatu usiku tulipomuachia kwa dhamana, taratibu nyingine
zinaendelea na tutawajulisha pindi tukapozikamilisha," amesema
Msigwa amekuwa mtuhumiwa wa nne kukamatwa akihusisha na matukio hayo
baada ya wiki iliyopita jeshi hilo kueleza kuwa linawashikiliwa
watuhumiwa watatu kwa mahojiano kutokana na kuhusika na tukio la kuchoma
nyumba ya aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM.
0 comments:
Post a Comment