Mbunge
wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa akishtakiwa kwa kesi mbili.
Katika
kesi moja anadaiwa kuchoma moto nyumba ya Mary Tesha aliyokuwa akiishi
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Alphonce Muyinga.
Mchungaji
Msigwa ambaye ni mshtakiwa wa saba katika kesi zote mbili amefikishwa
mahakamani leo Jumatano Januari 24,2018 baada ya kuripoti kituo kikuu
cha Polisi.
Katika
kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, David
Ngunyale, Wakili wa Serikali, Felix Chakla amedai kati ya Januari 5 na
14,2018 washtakiwa walipanga njama za kuharibu mali.
Pia
wanadaiwa Januari 15,2018 walibomoa nyumba ya Anjelus Mbogo aliyekuwa
diwani wa Mwangata aliyejiuzulu kutoka Chadema na kuhamia CCM.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema
Iringa Mjini, Leonce Marto; diwani mteule wa Viti Maalumu, Rehema Mbeta
na Patrick Madati.
Mchungaji Msigwa na wenzake wako nje kwa dhamana baada ya kila mmoja kusaini bondi ya Sh2 milioni.
Katika kesi ya pili, Mchungaji Msigwa na wenzake sita wanadaiwa kupanga njama ya kutenda uhalifu kinyume cha sheria.
Wakili Chakla mbele ya hakimu Ngunyale amedai Januari 17,2018 washtakiwa kwa pamoja walichoma nyumba ya Tesha aliyokuwa akiishi Muyinga.
Kwa
shauri hilo namba 7 la mwaka 2018, washtakiwa wanadaiwa Januari 17,2018
waliichoma moto nyumba hiyo iliyopo kata ya Kihesa katika Manispaa ya
Iringa.
Washtakiwa
walikana kosa na hakimu Ngunyale aliwaachia kwa dhamana baada ya kila
mmoja kudhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh3 milioni.
Mchungaji
Msigwa na wenzake katika kesi hizo wanawakilishwa na wakili wa
kujitegemea Anthony Rutebuka. Hakimu Ngunyale ameahirisha kesi hizo hadi
Februari 2,2018.
0 comments:
Post a Comment