Home » » 'ZINGATIENI SHERIA ZA UZAZI'

'ZINGATIENI SHERIA ZA UZAZI'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SERIKALI imewataka waajiri katika taasisi zake mbalimbali na zile zisizo za kiserikali kuzingatia na kulinda sheria zinazowalinda wanawake wanaojifungua kwa kuwapa likizo za uzazi.
Waajiri hao pia wametakiwa kuzingatia sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya unyonyeshaji duniani yaliyofanyika kitaifa wilayani Mufindi mkoani Iringa juzi, Katibu wa Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema kuwa mwanamke aliyejifungua mtoto mmoja anatakiwa kupewa likizo ya uzazi ya siku 84 na aliyejifungua watoto pacha anapewa likizo ya siku 100.
Alisema likizo hizo zinaambatana na malipo kamili ya mshahara na mama aliyejifungua anaweza kuchukua likizo yake ya mwaka akihitaji na mzazi aliyerudi kazini baada ya likizo ya uzazi anapewa ruhusa ya saa mbili kwa siku kwenda kumnyonyesha mtoto.
Pallangyo aliwaasa wadau wengine wanaojishughulisha na uuzaji wa maziwa mbadala ya watoto, mikoa na halmashauri zote kujua na kufuata kanuni za kitaifa zilizotungwa chini ya sheria za mamlaka ya chakula dawa na vipodozi sura ya 219.
Alisema lengo ni kudhibiti uuzaji na usambazaji wa maziwa mbadala ya watoto pamoja na bidhaa zinazoambatana na vyakula vya watoto.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuelimisha wanafamilia na wanawake hasa wale ambao wanaiga tamaduni za kigeni za ulishaji watoto ambazo mazingira yake ni potofu.
Awali Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala mkoa, Ayubu Warioba, aliitaka jamii kuelimishana kwenye kaya kuhusu unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto katika ustawi na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Naye mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto la umoja wa mataifa (UNICEF) Tanzania, Paul Edwards alisema shirika hilo na wadau wengine wanalenga kuimarisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kama njia ya ufanisi na kuokoa maisha ya mtoto
  Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa