Home » » TIMU TATU ZAPIGWA TAFU MUFINDI

TIMU TATU ZAPIGWA TAFU MUFINDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
TIMU tatu za soka za Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa zimepata msaada wa seti moja ya jezi na mpira mmoja kwa kila moja na shilingi milioni 8.1 kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi ya Wilaya.
Timu zilizofaidika na msaada huo ni Boda Boda FC, Wambi Stars na Wamachinga FC zote za mjini Mafinga.
Msaada huo ulitolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, wakati akifungua shina la wakareketwa wa UVCCM Stendi Kuu ya Mabasi Mafinga, kwa lengo la kukikuza chama kwa njia ya michezo.
Akikabidhi msaada huo kwa nahodha wa timu hiyo, Josephat Mkini, Nchemba alisema michezo ina nafasi kubwa ya kuajiri vijana na ni jukumu la wadau kusaidia kukuza michezo yote Tanzania.
Aliwaomba wadau wengine kujitokeza kuisaidia timu mbalimbali za vijana kwa lengo la kukuza mchezo wa soka na ikiwezekana siku moja Wilaya ya Mufindi iwe na timu Ligi Kuu.
Katika kukuza mchezo wa soka, Nchemba alichangia sh milioni 5 wakati Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa, alichangia sh milioni 2 na yule wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola, alichangia sh 500,000.
Kwa niaba ya timu hizo, nahodha Mkini alimshukuru Nchemba kuonyesha uzalendo kwa kuzipiga jeki timu hizo katika kukuza soka la vijana Wilaya ya Mufindi.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa