WAWANAKE mkoani Iringa wametakiwa kuzitambua haki zao sambamba na
sheria za utawala bora ndani ya jamii katika kukabiliana na vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Dk. Cephas Mgimwa,
alitoa kauli hiyo jana wakati wa mafunzo juu ya haki za wanawake
yaliyoandaliwa na Kitengo cha Haki za Binadamu na Utawala Bora wa chuo
hicho kwa wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Alisema mwanamke anapaswa kupewa nafasi za kutoa michango yao katika
uamuzi mbalimbali ndani ya jamii, ikiwemo masuala ya ndoa, umiliki wa
mali na masuala ya mirathi.
Alisema mafunzo hayo ya utawala bora yamelenga kuwajengea uwezo
wanawake kufikia mifumo mbalimbali ya mahakama, ili kupata msaada wa
kisheria kwa lengo la kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazowakabili, zikiwemo kupigwa, kubakwa, kuachika na kunyimwa mirathi
kutokana na baadhi ya mila potofu katika baadhi ya makabila.
Mgimwa alisema kumekuwa na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii
nyingi za Kitanzania, hasa watoto na wanawake walioko ndani ya ndoa na
nje ya ndoa na kwa kukosa ufahamu wa sheria na haki za binadamu wengi
wao wameshindwa kupeleka malalamiko yao sehemu husika.
Mhadhiri na Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa chuo hicho, Dk. Mary
Livera, alisema binadamu wote ni sawa na hakuna tofauti ya mwanamke na
mwanaume katika kupata haki za msingi za binadamu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment