Home » » Matukio ya uvamizi wa mabenki wazipa hofu benki za vijiji (VICOBA)

Matukio ya uvamizi wa mabenki wazipa hofu benki za vijiji (VICOBA)

KUKITHIRI kwa wimbi la uvamizi wa majengo ya taasisi za kifedha nchini, kumezitia shaka benki za wananchi waishio vijijini - Vicoba, na hivyo kuomba msaada kwa serikali kuweka ulinzi madhubuti kwa benki hizo ikiwemo kujengwa kwa vituo vya polisi kila kata.
Wakizungumzia hofu yao ya fedha zao katika uzinduzi wa Vicoba vya kikundi cha Uamsho na Ulete vya Iringa vijijini, wanachama hao wamesema fedha zao zipo mashakani kwa kutokana na matukio ya uvamizi wa benki nchini kukithiri.
Benitho Kimuli mwanakikundi wa Muwimbi Vicoba, amesema matukio ya ujambazi wa kuvamia benki ni tishio kubwa kwao, kwa madai kuwa baadhi ya vikundi vingine havina akaunti katika benki na hivyo hulazimika kuweka fedha zao katika nyumba za viongozi wao.
Diwani wa kata hiyo ya Lumuli Charles Lutego amesema kuna haja kwa serikali kujipanga zaidi ili kuhakiki ulinzi kwa benki za wananchi wa vijijini ambazo sasa zimekuwa nyingi lakini hazipo salama kwa kukosekana kwa vituo vya polisi vya Kata.
Aidha ofisi ya mbunge wa jimbo la Kalenga Dr. Willium Mgimwa kupitia mwakirishi wake Johakim Mgimwa imetoa ahadi ya kuviwezesha vikundi hivyo viwili jumla ya shilingi Milioni 5 na laki 5, huku mwakirishi huyo akiwaasa wanavikundi hao kuwa wabunifu katika kukuza uchumi wao, na kujitolea kuchangia mahitaji muhimu ya kijamii.
Hata hivyo mratibu wa Vicoba mkoani Iringa Tisiana Kikoti amewataka wanachama hao kuwa waaminifu kwa kukopa kwa nidhamu na kurejesha madeni kwa wakati, ili kutoa nafasi ya wanachama wengine kupatiwa mikopo hiyo.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa