MIONGONI mwa watu 5,631 mkoani hapa waliopima afya
zao katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, watu 503 wamebainika kuwa
na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Akizungumza katika kikao cha utekelezaji wa
shughuli za ukimwi zilizotekelezwa na Kamati ya Kudhibiti Ukimwi mbele ya
baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Julai na Septemba,
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naibu Meya Gervas Ndaki, alisema kati ya
waliojitokeza kupima na kupata ushauri nasaha, wanaume walikuwa 2,712 na
wanawake 2,919.
Ndaki alisema kati ya watu 503 waliopima kwa hiari
na kukutwa na maambukizi, 188 ni wanaume na wanawake ni 315.
Alisema huduma ya kuzuia maambukizi ya vvu/ukimwi
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, wajawazito 1,009 walijitokeza na kupata
ushauri wa nasaha na kati yao, 104 walikutwa na maambukizi.
Ndaki alisema mapambano ya ukimwi
yanaambatana na huduma za tiba sahihi ya magonjwa ya ngono na jumla ya
watu 564, wanaume 178 na wanawake 386, walipata tiba sahihi ya magonjwa ya
ngono.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment