Home » » Familia ya Mwangosi yawajia juu polisi

Familia ya Mwangosi yawajia juu polisi




Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) kimezindua mnara wa kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi, huku familia ya marehemu ikitoa siku 14 kwa Jeshi la Polisi kurejesha vifaa vya marehemu vinavyoshkiliwa na jeshi hilo tangu siku ya tukio.

Wakati wa uzinduzi huo baadhi ya  wananchi waliohudhuria waliangua vilio wakati maelezo yakitolewa na viongozi wa Chadema kuhusu jinsi Mwangosi alivyouawa kinyama Septemba 2 mwaka jana kwa kulipuliwa na bomu.

Mnara huo uliozinduliwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema  umejengwa katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa na imeelezwa umegharimu Sh. 2,320,000 ambazo zimechangwa na Watanzania mbalimbali.

Wakati wa uzinduzi huo ambao ulikwenda sambamba na kuweka mashada ya maua, magari matatu ya polisi yaliyowekwa  bendera nyekundu yaliyokuwa na askari zaidi 20 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) yalikuwa eneo la tukio yakirandaranda.

Mdogo wa marehemu, Andrew Mwangosi akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao pia ulihudhuriwa na mjane, Itika Mwangosi, alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kurejesha kamera, kompyuta mpakato (Laptop) na kinasa sauti (tape recorder) ndani ya siku 14 ambavyo vinashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Andrew alisema Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi lilimwita mjane wa Mwangosi na kumkabidhi kamera tu lakini alikataa kupokea hadi vitu vyote viwepo na kuahidi kukabidhiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa