na Francis Godwin, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewataka wanahabari kulisaidia taifa katika zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi hilo.
Mkuu huyo wa mkoa, alitoa rai hiyo juzi mjini Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Mkoa wa Lindi na Mtwara.
“Sensa ina nafasi kubwa katika taifa, kwani litawezesha serikali kupanga bajeti kulingana na idadi ya wananchi, hivyo wanahabari saidieni kutoa elimu zaidi kwa umma,” alisema.
Dk. Ishengoma alisema ana matumaini kwa siku zilizosalia, zitatumika vema katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi.
Pamoja na hilo, washauri wakuu wa kaya kuweka kumbukumbu sahihi ambazo zitawezesha makarani wa sensa kupata taarifa sahihi katika kufanikisha zoezi hilo.
“Pia ni marufuku kwa makarani wa sensa kuomba posho kwa wananchi wanaokwenda kuwahesabu, wala kuongeza idadi ya maswali ambayo hayamo katika orodha ya maswali yaliyomo katika dodoso fupi ama dodoso refu,” alisema.
Katika semina hiyo, wanahabari walioshiriki walitoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Njombe na wenyeji Iringa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment