Home » » DC MUFINDI ATAKA MAELEZO YA MILIONI 15 ZA KIJIJI

DC MUFINDI ATAKA MAELEZO YA MILIONI 15 ZA KIJIJI



Na Mwandishi Wetu, Mafinga
*Mbunge naye kufanya ziara kijijini
MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Evalista Kalalu amewataka viongozi wa kijiji cha Magunguli, kilichopo Kata ya Kiyowela wilayani humo, kutoa maelezo ya Sh milioni 15 za malipo ya kibali cha kuvuna magogo katika shamba la Sao Hill lililopo wilayani humo.

Fedha hizo zinadaiwa kuwekwa katika akaunti ya mtu binafsi, ambaye ni diwani wa Kata ya Kiyowela, ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo na mfanyabiashara wa mbao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Magunguli, Camillus Suta alikiri fedha hizo kutokuingizwa katika akaunti ya kijiji chake, zikiwa ni malipo ya kibali cha uvunaji magogo ambapo serikali ilitaka kijiji kiuze kwa mtu yeyote mwenye mitambo ya kuchana magogo, ili fedha zitakazopatikana zifanye kazi ya maendeleo ya kijiji.

Badala yake mwenyekiti huyo wa kijiji alisema, fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti binafsi ya diwani wa kata ya Kiyowela, Peter Tweve, jambo lililozua mtafaruku mkubwa kwa wakazi wa kijiji ambao baadhi waliamua kugomea shughuli za maendeleo ya kijiji hadi wapewe maelezo zilipo fedha hizo.

Kufuatia hali hiyo Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji na Kata ya Kiyowela, Otavio Kalinga, alitoa amri kwa askari polisi wa kituo kidogo cha Mgololo kukamata wananchi wote wanaogomea shughuli za maendeleo kijijini hapo, ambapo Juni 1 mwaka huu, wananchi watatu waliotajwa kuwa vinara wa kuuliza maswali katika mikutano waliwekwa ndani.

Mapema mwaka jana, serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilitoa ‘ofa’ ya kibali cha kuvuna magogo yenye meta za ujazo 500 kwa vijiji 12, vinavyozunguka shamba la miti la Sao Hill na mkuu wa wilaya kuviwekea utaratibu vijiji vilivyopewa mgao huo, ili pesa hizo zisifujwe.

Mkuu wa wilaya hiyo alivitaka vijiji kuuza vibali kwa wafanyabiashara kwa kuwa havina mitambo ya kuchana magogo na kuwataka viongozi wa vijiji husika (wenyeviti na watendaji), kufungua akaunti za vijiji kabla ya kuuza vibali, ili pesa hizo ziwekwe katika akaunti lakini uongozi wa kijiji ulikaidi kufanya hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amesema amesikia taarifa za ukiukwaji huo wa maagizo yake, hivyo amewataka viongozi wa kijiji kutoa maelezo mapema kabla yeye kwenda kuzungumza na wananchi, kuhusu uamuzi utakaochukuliwa na serikali kwa makosa waliyofanya viongozi wa kijiji.

“Kwanza tumetaka maelezo kwanini hawakufuata utaratibu uliowekwa na je fedha hizo zipo wapi, ndipo nitakwenda kijijini hapo kuitisha mkutano wa hadhara na kuwafahamisha wananchi hatua tutakazochukua dhidi ya viongozi wa kijiji kama fedha hizo zitakuwa zimepotea” alisema DC Kalalu.

Naye Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola (CCM), alisema anakusudia kwenda kijijini hapo kupata maelezo ya wananchi kuhusu suala hilo.

“Natarajia kwenda huko kufuatilia suala hilo mapema iwezekanavyo, nitakwenda kukutana na wananchi kupata maelezo yao, naamini tutapata muafaka wa suala hilo,” alisema Kigola.

Diwani Tweve anayedaiwa kumiliki kibali hicho bila kulipa fedha kama ilivyoamuriwa na DC Kalalu, alisema viongozi wa kijiji wamekuwa wakichukua fedha hiyo kidogo kidogo kwake na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya kijiji.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa