Home » » UJENZI WA STENDI MTO RUAHA WAPINGWA

UJENZI WA STENDI MTO RUAHA WAPINGWA


Na Mawazo Malembeka, Iringa.
BODI ya Maji Bonde la Rufiji, imesisitiza kuwa msimamo wake wa kupinga ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi karibu kabisa na mto wa Ruaha mdogo,eneo la Igumbilo,uko palepale na imeitaka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutafuta eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa stendi.

Wajumbe wa Bodi hiyo ya Bonde la Rufiji yenye mamlaka ya kusimamia rasilimali ya maji na mazingira katika eneo la bonde la Rufiji wamebainisha kuwa endapo stendi hiyo itajengwa eneo hilo,itahatarisha maisha ya wakazi wa Manispaa ya Iringa pamoja na maeneo mengine kutokana na uchafu ikiwemo wa kemikali kama diseli na Petroli utakaokuwa unaingia mtoni.

Hata hivyo, kutoka hapa si zaidi ya mita mia moja, unapita mto wa Ruaha mdogo ambao ndiyo chanzo kikuu cha maji ya kunywa ya wakazi wa Manispaa ya Iringa na wengineo ambayo huchukuliwa kupitia chujio au Intake ya Mamlaka ya maji safi na taka ya Manispaa ya Iringa (IRUWASA).

Manispaa ya Iringa kwa upande wake,iliajiri mshauri kufanya tathmini ya athari za mazingira (EIA) kwa ajili ya ujenzi huo na zipo taarifa kwamba Waziri wa Maji ameshasaini cheti cha kuruhusu ujenzi kuendelea lakini wajumbe wa Bodi ya Rufiji wameahidi kuendelea na jitahada za kupinga ujenzi huo.

Jackson Makweta, mmoja wa wajumbe wa Bodi hii anasema ni vyema likatafutwa eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa stendi kwa sababu gharama ya kulipa fidia ni ndogo ikilinganishwa na gharama aa maisha ya wananchi huku Mkurugenzi Msaidizi rasilimali ya maji katika Wizara ya maji, Bibi Naomi Lupimo anasema hajawahi kuiona ripoti ya Tathmini ya Mazingira iliyofanywa na Mtaalam aliyeajiriwa na Manispaa ya Iringa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bibi Theresia Mahongo hakupatikana lakini taarifa zilizopo ni kwamba licha ya kutenga tu eneo hilo kwa ajili ya Stendi, Manispaa hiyo pia ilipata zaidi ya milioni 400/- kwa ajili ya kuuza viwanja vya biashara kwa njia ya mnada vilivyopo karibu na kiwanja cha stendi hiyo tarajiwa.
Blogzamikoa

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa