Home » » RC AWAONYA VIONGOZI

RC AWAONYA VIONGOZI

na Francis Godwin, Iringa
MKUU wa Mkoa (RC) wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amepiga marufuku viongozi kuwasumbua wananchi kwa michango katika kipindi hiki cha kuelekea katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 26.
Kiongozi huyo pia ametangaza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kiongozi atakayebainika kuomba fedha kutoka kwa wananchi pindi anapokuwa katika majukumu yake ya kuhamasisha zoezi la sensa.
Dk. Ishengoma alitoa agizo hilo jana alipozungumza na Tanzania Daima ofisini kwake na kusema katika kufanikisha zoezi hilo, amesimamisha michango yote ya maendeleo kwa wananchi ili kuwaondolea hofu.
Hatua ya mkuu huyo imekuja baada ya baadhi ya viongozi kudaiwa kupita kwa wananchi na kukusanya michango ya maendeleo, hivyo kuingiwa na hofu kuwa, yawezekana viongozi hao wakatumia siku hiyo ya sensa kuwakamata kwa kutolipa michango.
Alisema kuwa, ni vema kwa kipindi hiki cha kuelekea katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa, viongozi wa vijiji, mitaa, kata na wilaya, wakaacha mpango wa kupita kwa wananchi kuchangisha.
Dk. Ishengoma alisema kuwa, kazi kubwa ambayo viongozi wanapaswa kuifanya kwa sasa, ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.
Alisema, michango ambayo wananchi wanaweza kuendelea kuchangia ni ile ya kwao kama ya harusi na shughuli nyingine za kifamilia na si ya miradi ya kimaendeleo ya serikali.
Hata hivyo, mkuu huyo alisema baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwepo kwa mabalozi wa nyumba kumi kutaka fedha kiasi cha shilingi 500 (sio Iringa) kwa wananchi wanaowafikia wakati wa uhamasishaji.
Alisema, Mkoa wa Iringa umefanya uhamasishaji wa kutosha juu ya sensa na bado unaendelea na kampeni hiyo, hivyo amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu zoezi hilo kwani taarifa zote zitakuwa siri.
Aidha, alisema wote watakaofanya kazi ya sensa, watakuwa na vitambulisho pamoja na mavazi maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo.
Wakati huo huo, Dk. Ishengoma aliwataka wananchi wa Mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi katika sensa huku akiwataka watu wenye ulemavu kutofichwa kwani wanayo haki ya kuhesabiwa.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa