Home » » KWA UCHAFU HUU MAKAMBAKO, KWANINI MKOA WA NJOMBE USIWE WA MWISHO KWA USAFI KITAIFA?

KWA UCHAFU HUU MAKAMBAKO, KWANINI MKOA WA NJOMBE USIWE WA MWISHO KWA USAFI KITAIFA?



Makambako.
Kwa miaka mingi mkoa wa Iringa umekuwa ukisifika kwa usafi ambapo umekuwa ukishika nafasi za juu hasa tatu bora kitaifa. Hili limekuwa ni jambo la faraja na la kujivunia kwa wakazi wa mkoa huu kwani usafi ni jambo la msingi katika maisha ya binadamu.
Hivi sasa Njombe ambayo ilikuwa ni mojawapo ya wilaya ndani ya mkoa wa Iringa imepandishwa hadhi na kuwa mkoa ambao ndani yake kuna wilaya nne za Njombe, Ludewa Makete na Wanging’ombe.  Hivi sasa macho na maskio ya wengi nchini yatakuwa kuiangalia hii mikoa mipya inafanya nini na inaelekea wapi hasa ikizingatiwa kwamba bado ni mipya.
Wasiwasi wangu ni uwezekano wa Mkoa huu wa Njombe kuvunja rekodi na kuwa wa mwisho kwa Usafi  kutokana na uchafu uliokithiri katika maeneo mbalimbali hasa katika mji wa Makambako ulioko ndani ya Wilaya ya Njombe tena makao makuu ya mkoa.
Uchafu huu uliokithiri unasababishwa na Wananchi wenyewe na pia Mamlaka zenye jukumu la kuhakikisha mji unakuwa safi.

Tukianza na Wananchi kuwa chanzo cha uchafu ni pale ambapo wanakosa ustaarabu pindi wanapoenda kutupa taka kwenye maeneo maalumu ya takataka maarufu kama ‘dampo’  ambapo badala ya kutumbukiza takataka ndani wao hurusha nje ya dampo na hivyo kusababisha takataka hizo kuanza kuzagaa kwenye mitaa jirani na madampo hayo.
Mbali ya hilo wananchi hawajawa na mazoea ya kufanya usafi kwenye mazingira ya makazi yao hasa kwa kuondoa nyasi kipindi hiki cha mvua na hivyo kusababisha uchafu majumbani.
Kwa upande wa mamlaka husika wameshindwa kuenda na kasi sahihi ya kuondoa takataka kwenye maeneo ya kutupa takataka hali inayopelekea mara kwa mara takataka kurundikana zikiwa zimejaa hadi kupitiliza na hivyo kuwa kero kwa wananchi. Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na hivyo wananchi kujiuliza nini wajibu wa serikali na hivyo kuuona huu kama uzembe uliokithiri.
Rai kwa Wananchi na Mamlaka zinazohusika ni kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha kwamba usafi unazingatiwa  ili siku moja Mkoa wetu wa Njombe utangazwe kama Mkoa namba moja kwa Usafi kitaifa. Tunaamini kwamba hilo linawezekana endapo wilaya zote zitajitahidi katika hili.
Chanzo: Makambakokwetu

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa