Na Oliver Richard, Iringa
BAADA ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kukabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi zaidi ya Sh bilioni 1.4, Baraza la Madiwani wa limemvua madaraka Mweka Hazina wa Wilaya hiyo, Ferdinand Manyele.
Akisoma waraka wa Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Uswege
Kaminyoge, alisema sifa zinazotakiwa mtumishi kuwa mkuu wa idara zilionyesha Manyele hakidhi vigezo hivyo na kisha madiwani kuazimia kuwa mtumishi huyo hastahili kuwa mkuu wa idara hiyo ya fedha.
Alisema baraza hilo limeridhia kumshusha madaraka mweka hazina huyo kutokana na kutokuwa na vigezo vya kugombea nafasi hiyo.
“Nimeagizwa kutoka TAMISEMI nipatiwe mweka hazina mwingine kuanzia sasa ambaye atakuwa na sifa nzuri za kutunza fedha za miradi ya wananchi,” alisema Kaminyoge.
Aidha, alisema vyeti vya aliyekuwa mweka hazina huyo
vimeonekana kutokuwa na sifa ya kuwa katika ngazi hiyo, baada ya kuvileta mbele ya madiwani na kulazimika kuvuliwa madaraka aliyokuwa nayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbarali, Keneth Ndingo, alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma inazingatiwa kujenga imani na msingi wa utawala bora kwa wananchi.
“Lazima tujenge nidhamu ya matumizi ya fedha za wananchi na sheria lazima itachukua mkondo wake, azma ya Serikali ni kuona fedha za wananchi zinatumika kwa miradi ya maendeleo iliyokusudiwa nasi vinginevyo,” alisema Ndingo.
Tuhuma hizo za kifedha zilibainika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kuitisha baraza la dharura ambapo fedha nyingi za miradi ya maendeleo zilionekana kuingia katika halmashauri hiyo, huku taarifa zake zikiwa hazifahamiki na miradi mingi kushindwa kutekelezwa.
Kutokana na kitendo hicho, Kandoro alimwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kupata vyeti vya wakuu wote wa idara kwa ajili ya kutambua kama wana sifa na vigezo vya kutumikia Halmashauri hiyo.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment