Home » » MANENO YA MKUU WA MKOA WA IRINGA, MHE. DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB.), WAKATI AKIONGEA NA MAKUNDI MBALIMBALI YA KIJAMII OFISINI KWAKE TAREHE 30 AGOSTI, 2012

MANENO YA MKUU WA MKOA WA IRINGA, MHE. DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB.), WAKATI AKIONGEA NA MAKUNDI MBALIMBALI YA KIJAMII OFISINI KWAKE TAREHE 30 AGOSTI, 2012


· Ndugu Viongozi wa watu wenye ulemavu
· Ndugu wawakilishi wa wazee
· Ndugu Viongizi wa Dini
· Ndugu Viongozi wa Siasa
· Ndugu Waandishi wa Habari
Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:
Sensa ya Watu na Makazi itaanza usiku wa Jumamosi tarehe 25/ 8/2012 kuamkia Jumapili tarehe 26/8/2012. Ili kuhakikisha kuwa Watu wote wanahesabiwa na wanahesabiwa mara moja tu, zoezi hili litaendelea kwa siku saba. Watu wote waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani tarehe 25 kuamkia tarehe 26/8/2012 watahesabiwa.
Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:
Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya Watu wote waliopo nchini ambapo taarifa zao za kijamii na kiuchumi hukusanywa. Sensa pia hukusanya hali ya Makazi ya Watu hao. Serikali inafanya Sensa ili kupata taarifa zitakazosaidia katika kupanga, kufanya maamuzi, kusimamia na kutathmini sera na mipango ya maendeleo. Taarifa za Sensa pia hutumiwa na Sekta binafsi na jamii kwa ujumla katika shughuli za kila siku.
Hivyo, ni muhimu kwa wananchi kushiriki Sensa kwa sababu kupitia Sensa Serikali itafahamu mahitaji ya wananchi wa kila rika, mahali walipo na watu wenye mahitaji maalum.
Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:
Siku ya Sensa, karani wa Sensa atafika katika kaya akiwa na dodoso la Sensa na kuuliza maswali ambayo yatajibiwa na mkuu wa kaya au mwanakaya mwingine badala yake. Karani huyo wa Sensa atafika katika eneo la kuhesabia watu akiwa na kitambulisho na atakuwa amevalia sare maalum zitakazomtambulisha. Aidha, atakuwa ameongozana na kiongozi wa eneo unaloishi.
Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:
Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 1 ya Mwaka 2002 taarifa zote zitakazochukuliwa na karani wa Sensa ni siri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu. Karani wa Sensa atakula kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazokusanya wakati wa Sensa.
Ni wajibu wa kila mwananchi kujibu maswali ya Sensa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 1 ya Mwaka 2002 ili Serikali iweze kupata Takwimu sahihi.
Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:
Endapo una swali lolote kuhusu Sensa tafadhali usisite kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya na utajibiwa swali lako lolote.
SENSA KWA MAENDELEO JIANDAE KUHESABIWA.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa