Home » » DC GUNINITA AWAONYA MAOFISA KILIMO

DC GUNINITA AWAONYA MAOFISA KILIMO



Na Francis Godwin, Iringa
MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Gerard Guninita amewajia juu maofisa kilimo na mifugo katika wilaya hiyo, ambao wamekuwa wakishinda ofisini, bila kwenda maeneo ya vijijini kutatua kero za wananchi.

Kutokana na hali hiyo, amewaagiza maofisa kila mmoja kuwa na daftari ambalo linaonyesha idadi ya wakulima na wafugaji aliowatembelea, vinginevyo watakatwa mishahara yao.

Guninita alitoa agizo hilo jana, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kidabaga.

Alisema anashangazwa na hatua ya mabwana shamba wa wilaya hiyo, kutokuwa na taarifa sahihi juu ya wakulima, huku wengi wao wakihudumia mashamba yao.

Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya utaratibu wa maofisa mifugo kupokea rushwa ya nyama wanapofika kukagua nyama machinjioni.

Alisema Wilaya ya Kilolo, imekumbwa na ugonjwa wa homa ya nguruwe, lakini katika hali ya kusikitisha maofisa mifugo hawajachukua jukumu la kupambana na ugonjwa huo.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwake, iwapo maofisa hao wa mifugo na kilimo hawafiki katika maeneo yao.

Kuhusu elimu, Guninita alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na ukosefu wa mabweni.

Wakati huo huo, wananchi wa kata hiyo, wamesema wanasikitishwa na kitendo cha wazee na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kubaguliwa wakati wa kupewa matibabu.

Kufuatia malalamiko hayo, Guninita amepiga marufuku kuona ama kusikia wazee na watoto, wanaendelea kutozwa gharama za matibabu.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa