Home » » WALIMU IRINGA WAKACHA MGOMO, WAIGEUZIA KIBAO CWT, WATAKA TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZI YA MICHANGO YAO

WALIMU IRINGA WAKACHA MGOMO, WAIGEUZIA KIBAO CWT, WATAKA TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZI YA MICHANGO YAO

BAADHI
ya walimu wa shule za msingi mjini Iringa wamekigeuzia kibao Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) wakipinga mgomo wake wa walimu ulioanza nchini
kote leo na badala yake wametaka waelezwe kwanza mapato na matumizi ya
michango yao ya kila mwezi kwa chama hicho.



“Tunasikia
kuna majengo ya walimu yanajengwa nchi nzima, makatibu wa cwt
wananuliwa magari, sasa kuna mpango wa kuanzisha benki, lakini hatupewi
taarifa ya mapato na matumizi, na hata magari waliyopewa makatibu hayana
msaada kwa walimu ambao ndio wenye mali hata kama wakiumwa,” alisema
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mtwivilla,. Sidified Mapunda.






Alisema
mgomo huo unawapa umaarufu viongozi wa chama hicho na hauna maana
yoyote kwa walimu wa kawaida kwasababu taratibu za kuongeza mishahara ya
walimu hazina tofauti na za watumishi wengine wa umma.



Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi y a Wilolesi ambayo pia
walimu wake wote walisusia mgomo hu, George Kameka alisema kabla ya
kumgomea mwajiri wao, wanataka kufahamu tangu kutoka kwa chama chao
hicho cha wafanyakazi tangu walimu nchini kote waanze kukatwa asilimia
mbili kwa ajili ya kukichangia, mapato na matumizi yake yakoje.





Alisema
kuna taarifa zisizo rasmi kwamba CWT iko katika mstari wa mbele kudai
maslai ya walimu ili mishahara yao ikipandishwa na wao wapandishe
michango yao.



Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chemichemi  ambayo
ni moja kati ya shule zake chache ambazo walimu wake wamegoma,
Demetrius Mgohamwende alisema walimu wote 20 wa shule hiyo wamegoma.




“Kama
unavyoona nimebaki mimi kama kiongozi ninayetakiwa kulinda pia mali za
shule na walimu wachache walioko kwenye mafunzo kwa vitendo, lakini
walimu wangu wote 20 wamegoma, baadhi yao walikuja asubuhi wakasaini
kitabu cha mahudhurio baadaye waliotoweka,” alisema huku akionesha
wanafunzi waliokuwa wakicheza nje ya viunga vya shule hiyo badala ya
kuwa madarasani.






Alisema mgomo huo una madhara makubwa yatakayoonekana kwenye mitihani ikiwemo ile ya kitaifa.


Alisema
kuna haja kwa serikali kusikiliza kero za walimu hao na kuzifanyia kazi
kwa kuzingatia uwezo wake badala ya kila mara kulalamika kwamba haina
uwezo.


Hata
hivyo taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya walimu waliokataa kuingia
katika mgomo huo zimedai wanashindwa kufanya hivyo kwa hofu ya kufukuzwa
kazi huku wakiwa na madeni makubwa kutoka katika taasisi mbalimbali za
fedha.





Kaimu
Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa, Peter Mvilli alisema katika baadhi ya
vituo, zipo taarifa za mgomo huo kutokwenda vyema kama walivyotarajia.






“Kuna baadhi ya shule  walimu
wake hawajagoma, na hivi sasa nimelazimika kutembelea shule hizo ili
kujionea hali halisi, taarifa kamili kuhusiana na hali halisi ya mgomo
huu nitaitoa baada ya kutembelea shule hizo za msingi na sekondari,”
alisema huku akiwapongeza walimu walioingia katika mgomo.



Kuhusu
madai ya CWT kutoweka wazi kwa wanachama wake taarifa za mapato na
matumizi, Mvilli alisema wanayo majibu na watatoa taarifa rasmi kwa
wananchama wao kupitia taratibu zilizoainishwa kwa mujibu wa katiba yao.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa