Na Oliver Richard, Iringa
WANAFUNZI 4,000 wa shule za sekondari wamekatisha masomo kwa tatizo la mimba za utotoni, kutokana na kukosa elimu ya afya ya uzazi na ndoa za mapema.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Ofisa Mradi wa Utetezi wa Shirika la AMREF.
Alisema tatizo la mimba za utotoni limesababisha wanafunzi hao wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19, kukatisha masomo kwa kupata mimba pamoja na kuozwa katika umri mdogo.
Alisema kukosekana kwa elimu hiyo kwa vijana wengi pia kumesababisha vifo vya uzazi, vitokanavyo na mimba za utotoni na hata kuwapo kwa takwimu ya vifo 454 kati ya wajawazito 100,000 wanaojifungua.
Aidha, alisema hata ugonjwa wa fistula na magonjwa ya ngono takwimu zake zinapanda, kutokana na vijana wengi kujihusisha katika uhusiano wa kimapenzi pasipo kutumia kinga.
Alisema magonjwa ya zinaa yatokanayo na ngono zembe yanaongezeka kwa sababu ya kundi hilo la vijana kutokuwa na elimu sahihi ya matumizi ya uzazi salama.
“Tumepata takwimu ya wasichana 4,000 kukatisha masomo yao kwa tatizo la mimba au ndoa za mapema, lakini pia tumebaini utoaji wa mimba hatarishi, matatizo yanayochangiwa na kukosekana kwa matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango.
“Baadhi ya vijana wengi wakiwa katika uhusiano wa kimapenzi pasipo kutumia kinga yoyote na hivyo kuwa katika hatari hizo, iwe ni kupata mimba, kupata magonjwa ya zinaa, ugonjwa wa fistula na hata baadhi ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na umri wao kuwa mdogo,” alisema Mollel.
Alisema sababu hizo na nyingine nyingi zimekuwa zikichangia umasikini kwa kiwango kikubwa, kwa kuwa vijana hao ambao ni asilimia zaidi ya 60 nchini, hushindwa kufikia malengo yao waliyojipangia.
Aliwataka wazazi kuwapa vijana haki yao kuchagua njia sahihi ya afya ya uzazi, huku akihimiza kundi hilo la vijana kuitetea haki yao hiyo kwa ajili ya kupata huduma bora za afya ya uzazi.
Naye, Kaimu Meya wa Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki, aliwataka vijana kuitumia afya ya uzazi na jinsia ikiwa ni pamoja na kupata taarifa hizo pasipo kuvunja maadili.
Alisema kiasi cha asilimia 29 ya vijana hasa waishio vijijini walio na umri kati ya 15-19 wameshapata watoto kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa kufanya ngono zembe pasipo kutumia kinga.
Alisema wasichana hususan waliopo shuleni wanapata ukimwi, magonjwa ya zinaa na mimba kutokana na kukumbwa na matukio mbalimbali likiwamo la ubakaji.
Aliema hata matumizi ya dawa za kulevya ni moja ya changamoto zinazochangia kuwapo wa matukio hayo, yanayowaangamiza vijana wengi huku baadhi yao wakiingia katika makundi mabaya na tabia nyingi hatarishi.
Mtanzania
0 comments:
Post a Comment