JITOKEZENI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI KUPIGIA KURA

“ Hakikisheni hizi siku 4 zilizobaki za Uandikishaji Wapiga kura kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wananchi wanajitokeza kwa wingi ili kuandikishwa katika daftari na waweze kutumia haki yao ya msingi tarehe 27 Novemba kuchagua viongozi wanaowataka na mawakala wa vyama vya siasa wanachama wenu hakikisheni wanaandikishwa katika Daftari asibaki hata mwananchi mmoja hajaandikishwa Mwenye sifa ya kuandikishwa”

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa OR- TAMISEMI Bi. Angelista Kihaga alipotembelea baadhi ya vituo vya Uandikishaji wapiga kura katika Halmashauri Ya Mji Mafinga lengo likiwa ni kuona hali ya Uandikishaji Daftari la Wapiga kura na kuhamasisha zoezi kwa kuongea na mawakala wa vyama vya Siasa, Wasimamizi Wasaidizi Ngazi ya Wilaya, Kata Mitaa na wananchi katika vituo alivyopitia.

Amesema zimebaki siku 4 za kuandikishwa hivyo hamasa iongezeke ili wananchi waweze kujiandikisha kwa wingi na waelekezwa kuwa bila kujiandikisha katika daftari hili hataweza kupiga kura tarehe 27 Novemba 2024, kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hata kama ana kadi ya Mpiga kura bila kujiandikisha katika daftari hataweza kupiga kura siku ya tarehe 27.

Bi Kihaga akiwa ameambatana na Viongozi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ngazi ya Mkoa wa Iringa amesomewa taarifa ya hali ya Uandikishaji kwa Halmashauri ya Mji Mafinga na Msimamizi wa Uchaguzi Mji Mafinga Bi. Fidelica Myovella ambaye amesema Uhamasishaji Unaendelea kupitia, radio, gari  za matangazo, madhehebu ya Dini, Mabonanza , Mikutano ya Hadhara elimu nyumba kwa nyumba.

Halmashauri ya Mji Mafinga ina jumla ya vituo 110 vya kuandikisha daftari la wapiga kura katika kata 9 zilizo katika Halmashauri ambapo zoezi la Uandikishaji daftari la wapiga kura kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kumalizika tarehe 20/10/2024

Imeandaliwa na 
Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mji Mafinga


USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Fidelica Myovella ameendelea na kusimamia Miradi ya Maendeleo kwa kuhakikisha inakamilika kwa Ubora wa fedha zinazotumika na kwa wakati.

Akiwa ameambatana na baadhi ya Wakuu wa Idara akiwepo Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Stephen Shemdoe leo tarehe 14/9/2024  Bi. Myovella amesimamia na kutembelea Ujenzi wa bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari JJ Mungai ambapo ujenzi upo hatua  lenta.

Aidha amekagua Ujenzi wa vyumba vitatu  vya madarasa katika Shule ya Msingi Kilimani ambapo maadalizi ya Upauaji yanaendelea.

Akiwa katika zoezi hilo la Usimamizi wa Miradi hiyo amewaagiza Idara husika zinazotekeleza Miradi hiyo kuwa karibu na mafundi ili kubaini changamoto yoyote inapotokea ili itatuliwe kWa haraka na Miradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa.

Wakati huo huo Bi Myovella amekagua ujenzi unaoendelea katika Shule ya Msingi Ifingo, ujenzi  wa vyumba viwili vya darasa ambapo ujenzi upo hatua ya kupaua na Ujenzi wa nyumba ya mwalimu 2 in 1 katika Shule ya Sekondari ya Ndolezi ambayo ipo hatua ya lenta.

Aidha amepongeza kwa kasi na ubara wa Miradi inayoendelea.

Imeandaliwa na Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Mafinga TC


TASAF YAMUWEZESHA MNUFAIKA MWENYE UONI HAFIFU KULETA BIDHAA KATIKA MAONESHO YA NANE NANE MBEYA 2024.

Na Sima Bingileki
Afisa Habari Mafinga Tc

“ Kwa kweli tunaishukuru Serikali  ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan kipitia TASAF tumeweza kushiriki Maonesho haya ya Nane Nane Jijini Mbeya kwani tumeleta majiko ya kupikia ya udogo tuliyoyafinyanga wenyewe,Hatujawahi kuwaza kuwa kuna siku na sisi tutafika Mbeya kwenye Maonesho haya na kuleta bidhaa zetu , Tunaishukuru sana Serikali”

Kauli hiyo imetolewa na Wanufaika wa TASAF kutoka katika Halmashauri ya Mji Mafinga wilaya ya Mufindi Bi Roida Mgwale(40) Mkazi wa Rungemba na Bi Honorina Nyongole(40) Mkazi wa Rungemba Mafinga mwenye Uoni Hafifu na mfinyanzi wa vyungu na majiko ya Udongo.

“Mimi nilikuwa na hali duni sana, kwa sasa nimekuja na majiko ya udongo 12 yangu mwenyewe na ninasomesha watoto, ninafuga na nina kuku 30 na ninakikundi naweza kununua hisa na udongo wa kutengenezea majiko mwenyewe. Nina uoni hafifu lakini TASAF kwa kweli wameweza kubadirisha maisha yangu na familia yangu” Honorina Nyongole Mnufaika

Naye Bi. Roida Ngwale(40) Mmoja
Wa wanufaika wa TASAF na mfinyanzi wa Vyungu na Majiko ya udogo amesema amewezeshwa na TASAF na amekuja na majiko30 pia anafuga kuku wa kienyeji, kusomesha  watoto na kilimo.

Halmashauri ya Mji Mafinga inashiriki maonesho ya Nane Nane Jijini Mbeya katika Viwanja vya John Mwakangale 2024 na kupitia Kitengo cha Maendeleo ya Jamii wanufaika wa TASAF  wawili Bi.Roida Ngwale na Bi.Honorina Nyongole wameweza kushiriki na kuonyesha bidhaa zao.

IMEANDALIWA NA SIMA MARK BINGILEKI
AFISA HABARI MKUU- MAFINGA TC

 

MRADI WA SLR WATENGA EKARI 28,000 UREJESHAJI UOTO WA ASILI

Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) imetenga ekari 28,000 za misitu ya jamii iliyopo katika vijiji vya Halmashauri saba (07) kwa ajili ya urejeshaji wa uoto wa asili.

Hayo yamebainishwa Julai 31, 2024 Mkoani Iringa na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa mahojiano na waandishi wa vyombo vya habari katika kikao cha siku moja cha kamati ya kitaifa ya usimamizi wa mradi kilichopokea taarifa ya mradi huo.

Dkt. Mapunda amesema tangu kuanza kwa mradi mwaka 2021, wataalamu walibainisha baadhi ya maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri zinazotekeleza mradi ili kuonesha juhudi na hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika urejeshaji wa uoto wa asili.

“Moja ya eneo ambalo tunaweza kujivunia kwa sasa katika mradi ni urejeshaji wa uoto wa asili…kati ya vijiji 54 vya mradi tuna vijiji ambavyo kwa sasa suala la uoto wa asili limeleta manufaa manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Mapunda.

Ameongeza kuwa kupitia mpango wa urejeshaji, baadhi ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji, huduma za mifumo ikolojia pamoja na shughuli za kilimo mseto.

Aidha Dkt. Mapunda amesema kupitia uhifadhi misitu jamii, mradi umewezesha shughuli endelevu na wezeshi ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa na kusaidia uhifadhi wa mazingira na kufanya usimamizi wa rasilimali zilizopo na kuandaa mpango matumizi bora ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kidunia ya kurejesha ekari Milioni 2.5 za uoto wa asili nchini ifikapo mwaka 2030.

Kuhusu vipaumbele vya bajeti ya mradi kwa mwaka 2024, Dkt. Mapunda amesema jumla ya vipaumbele vitano vimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mradi ambapo moja ya kipuambele hicho ni usimamizi wa biashara ya kaboni.

Ametaja vipaumbele vingine ni kuwezesha wakulima kutekeleza shughuli za miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ufugaji endelevu, kuhamasisha shughuli mbadala za kiuchumi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya shughuli za uzalishaji mali.

Kwa upande wake Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Doyi Mazenzele amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuweka mikakati ya pamoja kwa kuendelea kuhimiza jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa bioanuai ambazo zinachangia upatikanaji wa huduma ikolojia.

“Tumeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wananchi na wasimamizi wa miradi katika maeneo ya halmashaur” amesema Mazenzele.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Robert Masunya amesema Halmashauri hiyo imeendelea na juhudi mbalimbali za uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili kwa kuhimiza shughuli wezeshi zisizoharibu mazingira ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tumeendelea kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinapewa kipaumbele katika maeneo yote ndani ya Halmashauri ambayo yanatekeleza mradi kwa ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuhamasisha wananchi kutunza maeneo hayo" amesema Masunya.

Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unatarajia kukamilika mwaka 2025 na kunufaisha jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54. Halmashauri zinazonufaika na mradi ni Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.


 

USAJILI WA WAKULIMA KIDIJITALI WAFIKIA ASILIMIA 64.7

Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga.  Usajili wa wakulima kidijitali katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga umefikia asilimia 64.7, taarifa kutoka Idara ya Kilimo ya  Halmashauri hiyo inaonesha.

Taarifa kutoka idara hiyo inaonesha kuwa tangu zoezi la usajili lianze katika msimu wa kilimo wa 2022/23, tayari wakulima 23,222 kati ya 35,876 wamejisajili katika mfumo huo wa kidijitali.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Dkt. Kung’e Nyamuryekung’e Ijumaa ya Julai 26 alisema kuwa kwa kujisajili kidijitali, wakulima wataweza kupata huduma mbalimbali kiurahisi.

Alisema miongoni mwa huduma ambazo wakulima watapata kupitia kanzidata ya usajili ni mbolea za ruzuku, ugani na taarifa za masoko.

Sanjari na faida hizo, usajili wa wakulima kwenye mfumo, utaiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.

“Kwa kujisajili katika mfumo wa kidijitali mtaweza kununua mbolea kwa bei nafuu, mtaongeza uzalishaji na kuboresha maisha yenu na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,” alisema Dkt. Nyamuryekung’e.

Sekta ya kilimo ambayo ndio muhimili wa uchumi wa Tanzania, kwa mujibu wa taarifa kutoka wazara ya Kilimo, mwaka jana iliajiri asilimia 65.6 ya nguvu kazi ya Taifa na kuchangia asilimia 26.5 kwenye pato la Taifa.

Ni katika muktadha huo, Dkt. Nyamuryekung’e aliwasihi wakulima wa Mji Mbinga ambao bado hawajajisajili kwenye mfumo wa kidijitali, wafanye hivyo ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na Serikali na hivyo kuongeza mchango wao kwenye uchumi wa nchi.

Alisema zoezi la usajili, ambalo ni bure, linafanywa na maafisa kilimo wa vijiji au kata.

Taarifa zinazohitajika, alieleza, ni kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, mahali shamba lilipo, aina ya mazao yanayo limwa na ukubwa wa shamba.

Katika mazingira ambayo kilimo ndio sekta kuu ya uchumi, maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, yanategemea zaidi ufanisi katika sekta hiyo.

Na ndio maana serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira ya dhati ya kufanya mapinduzi katika sekta hiyo.

Hii inadhihirishwa na kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh294.16 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh1.25 tirioni mwaka huu wa fedha.

Sehemu ya bajeti ya wizara inatumika kutoa ruzuku kwa wakulima ili waweze kununua mbolea kwa bei nafuu.

Hatua hii ni muhimu katika kuwezesha uzalishaji wenye tija na hivyo kuwa chachu ya kuongeza kipato kwa mkulima mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

 

ELIMU YA KUZUIA MOTO YATOLEWA KWA WAJUMBE SERIKALI YA KIJIJI CHA RUNGEMBA- IRINGA

Elimu ya kuzuia Moto imetolewa kwa Serikali ya Kijiji Cha Rungemba lengo likiwa ni kutoa tahadhari ya moto hasa katika kipindi hiki cha Kiangazi ambacho kina upepo mkali na wananchi wanasafisha mashamba kwaajili ya kilimo.

Akizungumza Mkuu wa Kitengo Cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Ndugu. Demitrius Kamtoni akiwa ameambatana na Wataalumu kutoka kitengo hicho amesema
Ni muhimu vibali kutolewa na Serikali za vijiji husika kwa  mwananchi anayetaka kusafisha shamba kwa njia ya moto ili tahadhari zote za Moto zichukuliwe

Aidha Ndugu Kamtoni amesema Elimu nyingine iliyotolewa kwa wajumbe hao wa Serikali ya Kijiji cha Rungemba ni:-
-Sheria ya Udhibiti wa Moto
-Taratibu za Uchomaji Moto
-Uhifadhi wa Mazingira
-Utawala Bora wa Maliasili
-Ufugaji wa Nyuki na Vikundi vya Ufugaji Nyuki.

Elimu ya kuzuia moto, Utunzaji wa Hifadhi ya Mazingira na Maliasili itaemdelea kutolewa katika Kata zote za Halmashauri ya Mji Mafinga kwenye ngazi ya Kijiji na Mitaa kupitia Kitengo Cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira.

Imeandaliwa na Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini- Mafinga TC

 

MKURUGENZI SHULE ZA REALHOPE AKABIDHI KOMPYUTA TATU KWA HALMASHAURI YA MJI MAFINGA

“Lengo langu ni kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na Serikali hii na naahidi kuendelea kujitolea ili jamii iendelee kunufaika hasa katika Sekta ya Afya na Elimu,  kompyuta hizi 3 (Dell )zitarahisisha uwekaji wa takwimu na utunzaji wa kumbukumbu kidigitali hivyo kupunguza wagonjwa kukaa muda mrefu kusubiri huduma.”

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shule za Really Hope zilizopo Mji Mafinga Ndugu Dickson Mwipopo alipokuwa akikabidhi kompyuta 3 aina ya Dell zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 kwa Mkurugenzi Mji Mafinga Bi , Fidelica Myovella kwaajili ya matumizi ya Sekta ya Afya.
Akipokea compyuta hizo Mkurugenzi Mji Mafinga akiwa ameambatana na baadhi ya Wakuu wa Idara amesema  Msaada huu wa compyuta tatu utarahisisha utunzaji bora wa kumbukumbu na kuweka takwimu Sahihi kwa njia ya kidigitali, hivyo kupunguza kufanya kazi kwenye karatasi( paper work) kwani Serikali inahamasisha matumizi ya mifumo Sahihi iliyowekwa ili kuweka urahisi na huduma kwa haraka.

“ Serikali inathamini sana Wawekezaji ndio maana hata imeanzisha Wizara ya Uwekezaji lengo likiwa ni kuthamini juhudi za Wawekezaji na kuwapa mazingira bora ya kuwekeza bila urasimu, hivyo tunathamini juhudi zako kwani tunafahamu uwekezaji wako katika sekta hii ya Afya unaunga mkono jubudi za  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za Afya nchini, tunakuahidi kuzitunza kompyuta hizi na kuzitumia kwa lengo kusudiwa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya kompyuta hizo 3 zilizotolewa na Mkurugenzi wa Shule za Realhope Ndugu.Dickson Mwipopo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga Dkt. Bonaventura Chitopella amesema compyuta hizo zitawekwa Chumba cha Upasuaji na Maabara katika Hospital ya Mji Mafinga na moja itawekwa Zahanati ya Upendo kati Kata ya Upendo

Ndugu Charles Mwaitege Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu ametoa neno la shukrani kwa Mkurugenzi wa Realhope kwa Msaada wa Kompyuta 3 na kuahidi matumizi sahihi ya kompyuta hizi na kuleta mabadiliko sehemu zilizokuwa na changamoto ya upungufu wa vifaa hivyo.

Imeandaliwa na
Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mafinga TC

 

SALAMU ZA PONGEZI


Baraza la Waheshimiwa Madiwani, Timu ya Menejimenti na watumishi wote wa Halmashauri ya Mji Mafinga wanakupongeza  Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mheshmiwa Cossato Chumi  kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

HONGERA SANA
MAFINGA IPO SALAMA

NAFASI ZA KAZI HALMASHAURI YA MJI MAFINGA- 2024




TUWE MAKINI NA TAARIFA TUNAZOZITOA - MKURUGENZI HALMASHAURI YA MJI MAFINGA

“Mwaka huu 2024 ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo tuwe makini na taarifa tunazozitoa ofisini kwetu zisiende kutumika kwenye matumizi yasiyo sahihi na tutoe taarifa sahihi muda utakapo fika kwenye maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura.”
 
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi, Fidelica Myovella alipokuwa akizungumza na Watendaji wa Kata, Wakuu wa Idara na vitengo, Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu katika ukumbi wa JJ MUNGAI Mjini Mafinga.

Aidha amewataadharisha kutoa taarifa sahihi pale wanapotakiwa kutoa taarifa hizo kwa kibali maalumu ili kuhakikisha taarifa zinazoenda kwenye jamii hasa kipindi cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ziwe taarifa Sahihi.

Naye Afisa Mwandikishaji Uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura Ndugu, Charles Mwaitege amesema Halmashauri ya Mji Mafinga katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa itakuwaa na Vituo visivyopungua 145 vya Kupigia Kura.
“ Halmashauri ya Mji Mafinga katika Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura tunaendelea kujipanga na makadirio ni kuwa na wapiga kura 72,939 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 na vituo  visivyopungua 145 vya kupigia kura”

Halmashauri Ya Mji Mafinga ina Jimbo Moja la Uchaguzi la Mafinga Mjini, lenye Kata 9, Mitaa 30 Vijiji 11 na Vitongoji 50.

Imeandaliwa na
Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini- Mafinga TC

 

KITUO CHA AFYA UPENDO KUPUNGUZA MSONGAMANO KATIKA HOSPITATALI MJI MAFINGA

“ KITUO HIKI CHA AFYA UPENDO KIKIANZA KUTOA HUDUMA KITAPUNGUZA MSONGAMANO KATIKA HOSPITALI YA MJI MAFINGA NA HALI YA WANANCHI KUTEMBEA UMBALI MREFU KUFUATA HUDUMA ZA AFYA.TUNASHAURI KIANZE KUTOA HUDUMA”

Kauli hiyo imetolewa na Wajumbe ambao ni Waheshimiwa Madiwani wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya walipofanya ziara kukagua Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa chini ya Kamati hiyo. Miradi iliyotembelewa ni ukamilishaji wa Jengo la Maabara katika Kituo cha Afya Upendo na Jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Rungemba.

Akisoma taarifa ya Ujenzi wa Maabara katika Kituo cha Afya Upendo Mtendaji wa Kata ya Upendo Bi.Marry Luka amesema ujenzi wa Maabara ulianza tarehe 2/9/2023 baada ya kupokea fedha shilingi Milioni 50 kutoka Serikali Kuu, baadae Halmashauri ya Mji Mafinga kutoka katika Mapato yake ya ndani ikatoa shilingi Milioni 20 ili kukamilisha ujenzi wa Maabara hiyo.

Ameongeza kuwa kazi zinazoendelea ni uwekaji wa Milango, Meza za maabara, Masinki.

Waheshimiwa Madiwani wa Kamati hiyo wamempongeza Mkurugenzi Mji Mafinga Bi. Fidelica Myovella kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na Ushirikishaji wa Wataalamu, Watendaji wa Kata na kamati za Ujenzi katika Miradi hiyo. Aidha wameagiza ukamilishaji wa Maabara ufanyike haraka ili kituo kianze kutoa huduma kama ambavyo maelekezo ya Serikali yanataka.

Kata ya Upendo katika Halmashauri ya Mji Mafinga  ni moja katika ya Kata Tisa za Mji Mafinga ina jumla ya Mitaa Mitano na wakazi wasiopungua Elfu 25.

Imeandaliwa na
Sima Mark Bingileki
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Mafinga TC

 

ZIARA YA KIKAZI YA KAMATI YA UCHUMI, ELIMU NA AFYA HALMASHAURI YA MJI MAFINGA KUKAGUA MIRADI

Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya ya Halmashauri ya Mji Mafinga Imefanya ziara kukagua Mradi wa Ukamishaji wa Mabweni Mawili ya wasichana katika Shule ya Sekondari Changarawe iliyopokea Shilingi Milioni 67.7 kutoka Serikali Kuu kwaajili ya Ukamilishaji wa mabweni mawili.

Akitoa taarifa kwa Kamati hiyo Mkuu wa Shule ya Changarawe Mwalimu  Peter  Mbata amesema Halmashauri ya Mji Mafinga kupitia Shule ya Sekondari Changarawe ilipokea fedha kutoka Serikali kuu kwaajili ya Ukamilishaji wa Mabweni hayo mawili.

Amesema ukamilishaji huo umehusisha upakaji wa Rangi, uwekaji wa malumalu,utengenezaji wa Mifumo ya Maji na ukamilishaji unatarajia kukamila tarehe 14/7/2024. Mabweni hayo yanatumiwa na wanafunzi wa kike 240.

Wajumbe wameshauri ukamilishaji uende kwa haraka ili kuwaruhusu wanafunzi kuanza masomo kwani kwa kuwa na miundombinu bora shuleni inachochea kuongeza mori kwa wanafunzi kusoma.

Shule ya Sekondari Changarawe ina jumla ya wanafunzi 1284 na Inapatikana katika Halmashauri ya Mji Mafinga.

Sima Bingileki
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini

 
 

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa