CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kwa kishindo kampeni za Uchaguzi
Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Kimala wilayani Kilolo mkoani Iringa
huku Barthoromeo Kisoma, baba mzazi wa mgombea wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), akipanda jukwaani na kuwataka wapiga kura wa
kata hiyo wasimchague mwanaye.
Wakati CCM inawakilishwa katika uchaguzi huo na Amoni Kikoti, mkazi
wa Kijiji cha Uruti, Chadema imemsimamisha Tumson Kisoma aliyehamishia
makazi yake Iringa Mjini. Baba mzazi wa mgombea huyo wa Chadema alitoa
rai hiyo baada ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Kilian Myenzi
kumnyanyua katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo za CCM
zilizofanyika juzi katika Kijiji cha Kimala na kumtaka kuwasalimia
wananchi.
“CCM oyeeeeeee, CCM oyeeeee,” alisema mzazi huyo na kuwafahamisha
wananchi waliofurika katika mkutano huo kwamba mgombea wa Chadema ni
mwanawe, lakini hana uwezo wa kuwawakilisha wananchi wa kata hiyo.
Kisoma alisema kata hiyo inahitaji maendeleo ya kweli na mahali pekee pa
kuyapata ni kupitia CCM, hivyo kuomba wapiga kura wamchague mgombea wa
CCM, Amoni Kikoti.
Awali Myenzi ambaye pia ni sehemu ya familia ya Kisoma alisema Kata
ya Kimala inahitaji diwani wa CCM ili kutengeneza mnyororo mzuri wa
mawasiliano na Serikali ya CCM. Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa,
Christopher Magala aliwaomba wapiga kura wa kata hiyo kujihadhari na
matapeli wa kisiasa wanaobadili rangi za hoja zao kila kukicha. “Kabla
Rais Magufuli haijaingia madarakani hoja zao zilikuwa rushwa, ufisadi,
ubadhirifu wa mali za umma na nyingine nyingi.
Baada ya hayo yote kuanza kushughulikiwa katika awamu hii ya uongozi,
wamebadilika sasa wanatetea watu wanaojihusiha na vitendo hivyo, nchi
haihitaji viongozi wa aina hiyo,” alisema Magala. Naye Mjumbe wa Mkutano
Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Mufindi, Iringa , Jamhuri William
alisema; “sioni ni kwa namna gani, wananchi wa kata hii mtamchagua
mgombea kutoka katika chama kilichoshindwa vibaya katika Uchaguzi Mkuu
wa 2015.”
Aidha kada maarufu wa CCM, Asia Abdalla alisema Kikoti atashinda kwa
kishindo kwa sababu wapiga kura wanajua mengi yaliyofanywa na
yanayoendelea kufanywa na Serikali. Abdalla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya
ya Kilolo, alitaja miradi ya maendeleo ambayo Serikali ya CCM
imeitekeleza katika miaka miwili iliyopita na akasema mengi yanakuja.
Akimwombea kura, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto alisema;
“Kikoti ana sifa za kuwa msaidizi wangu kwani ni mwadilifu, mwaminifu na
mchapakazi, mchagueni.” Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Zainabu
Mwamwindi alisema Kata ya Kimala ni kata iliyoongozwa na CCM kwa miaka
yote itakuwa miujiza kama watakengeuka.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment