Home » » WANANCHI 4270 WAPATIWA ELIMU KUHUSU MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI VIJIJINI

WANANCHI 4270 WAPATIWA ELIMU KUHUSU MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI VIJIJINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Muwezeshaji wa Mafunzo kuhusu Mpango wa Matumizi bora ya ardhi kutoka Shirika la PELUM Tanzania, Josent Tesha akifafanua jambo kwa wananchi wa Kijiji cha Ugesa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa kuhusu manufaa na faida ya mpango huo hivi karibuni. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Pelum na kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Mwezeshaji wa Mafunzo kuhusu Mpango wa Matumizi bora ya ardhi kutoka Shirika la PELUM Tanzania, Simon Mbago akifafanua jambo kwa wananchi wa Kijiji cha Ugesa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa kuhusu manufaa na faida ya mpango huo hivi karibuni. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Pelum na kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

SHIRIKA la PELUM Tanzania kupitia Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika sekta ya kilimo (CEGO) limefanikiwa kutoa elimu ya mafunzo kuhusu Mpango wa Matumizi bora ya ardhi kwa wananchi4,270 kutoka Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Iringa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari hii Mjini Morogoro, Afisa Tathimni na Ufuatiliaji wa Shirika la PELUM Tanzania Frank Maimu alisema katika awamu ya kwanza shirika hilo lilitoa mafunzo kwa wananchi 3,070 na awamu ya pili wananchi 1200 na na tathmini yao ilibaini kuwa kuna uhitaji mkubwa wa wananchi wengine kupatiwa elimu hiyo. Maimu alisema kuwa, kupitia mradi wa CEGO unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), Shirika hilo lilihakikisha kuwa wananchi wanapatiwa elimu ya masuala ya ardhi kama njia mojawapo ya kuhakikisha mpango huo unakamilika kwa ridhaa ya wananchi wenyewe.

“Katika mafunzo hayo tunatoa elimu kupitia mada mbalimbali ikiwemo Mpango wa matumizi ya ardhi kijijini, haki za ardhi kwa wanawake, haki ya kupata, kutumia na kumilikia ardhi Tanzania, utatuzi wa migogoro ya ardhi Tanzania pamoja na utawala wa kidemokrasia katika Jamii” alisema Maimu.

Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo ya mipango ya matumizi ya ardhi vijijini, wananchi hao pia waliweza kuelimishwa njia mbalimbali za kutatua migogoro ya ardhi, kufahamu umuhimu na haki wa kumiliki ardhi kwa makundi mbalimbali pamoja na wananchi kuweza kusimamia Serikali zao kuanzia ngazi za vijiji.

Kwa mujibu wa Maimu alisema mbali na wananchi wa kawaida makundi mengine yaliyopatiwa mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kamati za maamuzi, mabaraza ya ardhi ya kijiji, mabaraza la kata pamoja na Halmshauri za vijiji.

Kwa upande wake Devota Winga kutoka kijiji cha Nchinila Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma anasema kupitia mafunzo yanayotolewa na Shirika la PELUM Tanzania ameweza kufahamu haki zake za msingi katika masuala ya ardhi ikiwemo sheria ya umiliki wa ardhi jambo ambalo halikuwepo katika jamii zao siku za nyuma

Naye Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Iduo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Bi. Ashura Elianaki anasema idadi ya kesi za migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiripotiwa katika Serikali ya Kijiji hicho kwa sasa imepunguakwani kwa sasa wananchi wengi wameweza kuelimika kupitia mafunzo ya Shirika la PELUM Tanzania.

“Wananchi wengi sasa wameweza kuelewa na kufahamu kwa undani wa sheria zinasemaje na na aina ya kesi zinazopaswa kutafutiwa suluhu na zipi zinapaswa kusuluhishwa na vyombo vingine kwa kuanza kusikilizwa na Baraza la Ardhi la Kijiji na sio Serikali ya kijiji”.alisema Elianaki.

Mbali na PELUM Tanzania kutoa mafunzo kwa wananchi wananchi 4,270 na kutekeleza Mpango wa matumiz ya Ardhi kwa vijiji vya mradi, Shirika hilo pia linatarajia kutoa hatimiliki za kimila 4883 kwa vijiji 25 vya awali ambavyo vimeshafanyiwa Mpango wa matumizi ya Ardhi.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa