Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wanafunzi wa chuo kikuu Iringa wakiwa katika mgomo leo |
Askari polisi wakiwa chuo kikuu cha Iringa leo |
Viongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa wakiwatuliza wenzao leo |
Ulinzi ukiwa imara katika chuo hicho leo |
Viongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa na wale wa chuo wakielekea kuzungumza na wanafunzi waliogoma |
Mkuu wa chuo kikuu ya Iringa Prof Joshua Madumulla akizungumza na wanafunzi hao |
mmoja kati ya wanafunzi wa chuki kikuu cha Iringa akitoa malalamiko yake dhidi ya bodi ya mikopo kwa kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Angeline Mabula leo |
Kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Mabula akizungumza na wanafunzi hao |
Na FGBlog |
WAKATI migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ikiendelea kuibuka wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa leo wamefanya mgomo wa kutoingia madarasani wakishinikiza uongozi wa bodi ya mikopo nchini kuwapa fedha zao za Kijikimu ambazo wamecheleweshewa kwa zaidi ya siku 63 sasa.
Huku wakitaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati uzembe wa bodi ya mikopo na hazina kwa kuwawajibisha watendaji wabovu katika idara hizo mbili kwa kosa la kushindwa kutimiza wajibu wao
Wakizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama iliyoongozwa na kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Angeline Mabula ambae ni mkuu wa wilaya ya Iringa ,wanafunzi hao walisema kuwa jumla ya wanafunzi zaidi ya 2000 katika chuo hicho ambao wapo katika orodha ya kupewa mkopo wa Tsh 472,500 hadi sasa wameshindwa kabisa kuendesha maisha yao chuoni hapo baada ya serikali kupitia bodi ya mikopo kuwacheleweshea pesa zao .
Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo Michael Msuya alisema kuwa wanafunzi hao kabla ya kufikia uamuzi wa kugoma waliomba kibali kwa jeshi la polisi kwa ajili ya kufanya maandamano leo (jana) kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kufikisha madai yao ila hawakuweza kupatiwa kibali hicho .
" Tuliandika barua polisi kuomba kibali ila hatukupewa kibali ila tunashukuru uongozi wa serikali ya mkoa kufika chuoni hapa kutusikiliza madai yetu .......ukweli wanafunzi waliocheleweshewa mikopo yao wanaishi katika mazingira magumu na baadhi yao wamefukuzwa katika nyumba ambazo walipanga"
Alisema kuwa fedha ambazo kila mwanafunzi kwa siku alipaswa kupewa na bodi ya mikopo ni Tsh 7000 kwa siku ila cha kushangaza hadi sasa wiki moja na nusu imepita bila kupewa pesa hiyo hali iliyopelekea wanafunzi hao kuingia katika mgomo
Msuya alisema kuwa kawaida wanafunzi hao walipaswa kupewa pesa hiyo na bodi ndani ya siku 63 ila cha kushangaza ni baada ya siku hizo kumalizika bila kuingiziwa pesa hizo katika akaunti zao .
Hata hivyo Rais huyo alisema kuwa bodi hiyo ya mikopo inapaswa kuchunguzwa ili kuwa na viongozi watakaotimiza wajibu wao kwa wakati na kuepusha migomo ya mara kwa mara kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini huku akiwashauri viongozi wenzake wa vyuo vingine kabla ya kuingia barabarani kuandamana basi kutumia njia nzuri ya kukaa na viongozi wa serikali ili kuepusha vurugu zisizo na tija .
Alisema ni kweli hali ya maisha kwa wanafunzi ni mbaya zaidi kutokana na kukosa pesa hizo ila busara zinapohitajika ni vema kutumika .
Huku Bw Kenani Kihongosi katibu wa TAHALISO na waziri mkuu wa chuo kikuu cha Iringa alisema kuwa chimboko la migomo hiyo ni bodi ya mikopo kwani vyuo vingi nchini havijapata pesa hizo na hivyo kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi wachache serikali ndio umepeleka migomo katika vyuo .
Alisema kuwa kumekuwepo na uzembe wa uingizaji wa fedha hizo na kuwa ni vizuri serikali kuondoa aibu hiyo ya migomo serikali kutoa pesa haraka kwa wanafunzi ili kuepusha migomo hiyo na iwapo watashindwa kupewa pesa hizo basi serikali ya wanafunzi nchini itatangaza mgomo kwa vyuo vyote nchini.
Pia alishangazwa na hatua ya bodi ya mikopo kutoa pesa kwa vyuo baada ya kufanya mgomo jambo ambalo alisema ni hatari kwa Taifa kwani ilipendeza bodi ya mikopo kuwabana hazina ili kuingiza fedha kwa wakati ili kunusuru mikopo .
Kuhusu madai ya baadhi ya watu kuhusisha migomo hiyo kisiasa alisema kufanya hivyo ni kuwakosea wanafunzi hao ambao ni haki yao kupata mikopo ila kama siasa basi inafanyika katika bodi ya mikopo na Hazina ambao wanawacheleweshea pesa wanafunzi hadi kusababisha maandamano vyuoni .
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa chuo kikuu cha Iringa Profesa Joshua Madumulla ,afisa mikopo wa chuo hicho Bi Marcela Mtewele alisema kuwa uongozi wa chuo hicho umefanya jitihada kubwa kuwasiliana na bodi ya mikopo toka wiki mbili zilizopita na kuwa majibu yao ni kuwa wao bodi ya mikopo kutowekewa pesa na hazina .
Japo alisema hadi jana na leo asubuhi wamejulishwa na bodi ya mikopo kuwa pesa hizo zipo na wakati wowote wataingiziwa katika akaunti zao.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Mabula mbali ya kuwapongeza wanafunzi hao kwa kutoandamana mitaani na kutulia ndani ya chuo hicho bado alisema alipokea barua kutoka kwa viongozi wa serikali ya wanafunzi ambao waliomba kukutana nae ofisini japo hawakuweza kufika kwa kuutaka uongozi wa serikali ya mkoa kufika chuoni hapo .
Aidha alisema kuwa lengo la serikali si kuona wanafunzi hao wanapata shida pindi wanapokuwa vyuoni ila kinachokwamisha ni hatua ya fedha kutolewa kwa awamu awamu kwa vyuo hivyo na ndio sababu ya baadhi ya vyuo hadi sasa vimekwisha pata pesa hizo.
Bi Mabula alisema tayari serikali ya mkoa wa Iringa imefanya mazungumzo na kaimu wa bodi ya mikopo pamoja na kamishina wa bajeti na wote wamekubali kulishughulikia suala hilo na kuwa ndani ya wiki hii chuo hicho watakuwa wamepata pesa zao.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) muda wote wakiwa wamezunguka chuo hicho na baadhi yao wakiwa ndani ya chuo kuimarisha ulinzi japo muda wote toka saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana uongozi wa serikali ya mkoa ulipofika chuoni hapo hali ilikuwa ni shwari na hakukuwa na vurugu zozote chuoni hapo.
Wakati huo huo wanafunzi zaidi ya 8 wamekamatwa na jeshi la polisi baada ya kufanya vurugu kwa kufunga barabara kuu ya Iringa - Dodoma kwa mawe kupinga majibu yaliyofikiwa kati yao na na viongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa .
Wanafunzi hao walifikia hatua hiyo ndani ya dakika takribani 20 hivi baada ya msafara wa kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa kuondoka chuoni hapo .
Hata hivyo uongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo umeeleza kushangazwa na hatua ya wanafunzi hao kwenda kufunga barabara wakati tayari suala lao likiwa linashughulikiwa na kwa kauli moja kukubaliana na majibu ya serikali juu ya madai yao.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi alipoulizwa na mtandao huu wa www.matukiodadaima.co.tz kuhusiana na kukamatwa kwa wanafunzi hao alithibitisha kuwa ni kweli wapo wanafunzi ambao wanashikiliwa na polisi kwa kosa la kufanya vurugu katika barabara hiyo na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani .
CHANZO : MATUKIO DAIMA BLOG
Share this article :