Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Biometric Voters Registration (BRV).
Uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu
la Wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voter Registration
(BVR) umekwama kuanza mkoani Iringa kutokana na sababu mbalimbali
ikiwamo kucheleweshwa kwa vifaa.
Akizungumza na NIPASHE jana kwa niaba ya Ofisa Uandikishaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Gabriel Msunza, alisema uandikishaji
ulipangwa kuanza leo, lakini kutokana na changamoto hiyo wameamua
kusogeza mbele hadi Jumatano ijayo.
Msunza alisema hadi sasa wamepokea BVR 39 na vifaa hivyo ni kwa
ajili ya mafunzo kwa waandishaji wasaidizi na kwamba wanasubiri
utaratibu mwingine kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
“Tunawasubiri tume leo (jana) wakishafika tutakaa nao na kujadili
na baadaye watatupatia tarehe rasmi ya kuanza uandikishaji baada ya
waandikishaji wasaidizi kupata mafunzo ya namna ya kutumia mashine
hizo.
Alisema Manispaa ya Iringa wanatarajia kuandikisha zaidi ya wapiga kura 79,089.
Wakati huo huo, Wilaya ya Lindi Vijijini, mkoani hapa, imepokea
vifaa vya uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration
(BRV).
Vifaa hivyo vitatumika kuandikisha wapigakura kwa ajili ya uchaguzi
mkuu wa mwaka huu. Hayo yameelezwa na ofisa Uchaguzi wa wilaya hiyo,
Musa Nkolovigawa, alipokuwa akitoa maelezo wakati wa semina ya mafunzo
ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapigakura. Nkolovigawa alivitaja
vifaa vilivyopokelewa kuwa ni BRV kiti 66, stendi za kamera, bahasha,
kofia, tisheti, mabegi ya kubebea vifaa na karatasi zitakazotumika
kujaza taarifa za mtu atakayefika kituoni kujiandikisha.
Alisema kupokelewa kwa vifaa hivyo ni moja ya ushahidi kuwa kazi ya
uboreshaji wa daftari hilo itaanza wiki hii kama ilivyopangwa.
Nkolovigawa alisema kazi ya uandikishaji imepangwa kuanza leo kwa
utaratibu wa kanda nne, ikimaanisha kata zote za majimbo yote mawili ya
Mtama na Mchinga.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda,
aliwataka maofisa waandikishaji ngazi ya kata wanakuwa makini kutokana
na uandikishaji kuwa ni suala nyeti na muhimu kwa kwa mustakabali wa
Taifa. Uandikishaji wa wapigakura katika Halmashauri ya wilaya hiyo
utaanza leo na kukamilika Mei 28, mwaka huu.
Imeandikwa na George Tarimo, Friday Simbaya, Iringa na Said Hamdani, Lindi
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment