MFANYABIASHARA maarufu wa mjini Iringa, Geofrey Mungai, amewawezesha watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Children’s Home kusherehekea vizuri sikukuu ya Krismasi na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2015 kwa kuchangia zaidi ya Sh milioni 2.
Kiasi hicho cha fedha kimewawezesha watoto hao zaidi ya 39 wa kituo hicho kilichopo Mkimbizi mjini Iringa, kupata vyakula mchanganyiko na vinywaji baridi wakati wa Krismasi na nguo mpya walizovaa siku hiyo na watakazovaa Januari 1, 2015.
“Watoto hawa wanawakilisha kundi kubwa la watoto wenye sifa kama zao ambao kama jamii inayowazunguka haitakuwa jirani nao, kuwaonesha upendo na kuwapa misaada muhimu wanayohitaji, ndoto zao za maisha zinaweza kupotea,†alisema Mungai baada ya kutoa msaada huo.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkewe, Sarah Mungai, Mungai alisema baada ya kusaidia watoto hao kwa miaka kadhaa iliyopita, hivi sasa anaona jambo hilo kama wajibu wake anaotakiwa kuutekeleza kila mwaka.
“Nimejifunza mahitaji ya watoto hawa na moja ya hitaji lao muhimu ni upendo kutoka kwa watu wanaowazunguka kwa kuzingatia kwamba hawakupenda wazaliwe katika mazingira waliyonayo,†alisema na kutoa mwito kwa wengine kushiriki kutatua changamoto zao.
Akimpongeza Mungai kwa mchango wake kwa watoto hao, Mkurugenzi wa shirika la Daily BreadLife Tanzania linaloendesha kituo hicho, Mchungaji Mpeli Mwaisumbi alisema: “Wakipata mahitaji yao muhimu na haki zao za msingi, watoto hawa, wenye malengo mengi katika maisha yao, wanaweza kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa hili.
“Kwa bahati mbaya wakiwa katika mazingira kama haya wengi wetu tunadhani kati yao, hatuwezi kupata wasomi waliobobea na wanaoweza kushika nafasi nyeti za uongozi katika Taifa hili,†alisema.
Alisema ili watoto hao wafikie ndoto walizonazo katika maisha yao ni muhimu wakapata mahitaji yao mbalimbali kama ilivyo kwa watoto wengine.
Alitoa mwito kwa wenye nafasi kuwakumbuka kwa kile alichosema wanapofanya hivyo wanaongezewa baraka za Mungu.
Tangu kuanzishwa kwake mkoani Iringa 2004, mbali na kuendesha kituo hicho cha watoto yatima, shirika la Daily Bread Life Tanzania linaendesha pia kituo cha watoto yatima cha Nzihi chenye watoto 24 huku likitoa msaada kwa watoto 241 walio nje ya shule katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Iringa.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment