Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
UVUVI
haramu umeelezwa na wananchi wa vijiji vya Mbweleli na Makatapola,
Iringa Vijiji mkoani Iringa kuhatarisha uwepo wa baadhi ya samaki
wanaopatikana katika bwawa la Mtera.
Samaki hao ni pamoja na Ngalala, Pelege Dungu, Ngogo na Ngobole ambao ukubwa wake ni chini ya inchi tatu.
"Umaskini ni moja ya
sababu inayowafanya wavuvi wakiwemo wale wanaotoka katika vijiji hivi
kujiingiza katika uvuvi haramu ili wakabiliane na changamoto za
kiuchumi," alisema mkazi wa Kijiji cha Mbweleli, Jenirosa Mbunda.
Hayo yalielezwa katika
mafunzo ya siku tatu yaliyofanywa kwa wananchi wa vijiji hivyo na Asasi
ya Maendeleo ya Mazombe Mahenge (MMADEA) inayoshirikiana na Taasisi ya E
Link Consult Ltd hivi karibuni mkoani hapa, kutoa elimu ya mabadiliko
ya tabia nchi, kwamba wizi wa nyavu na ukosefu wa elimu ni sababu
nyingine inayosababisha uvuvi haramu katika bwawa hilo.
Ofisa Uvuvi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Nelson Mbawala alisema katika mafunzo
hayo Sheria ya Uvuvi inaruhusu samaki wanaotakiwa kuvuliwa wawe na
ukubwa wa nchi tatu na kuendelea.
"Ikitokea mvuvi akavua
samaki ambaye hatakiwi kuvuliwa kwa mujibu wa sheria anatakiwa
kumrudisha bwawani hata kama amekufa," alisema Mbawala.
Alisema, uvuvi wa
kutumia makokoro unafanywa na wavuvi wengi katika bwawa hilo kwa sababu
unaelezwa kuwanasa samaki wengi kwa muda mfupi ikilinganishwa na ule
halali wa kutega.
Mbali na kuwamaliza
samaki katika bwawa hilo, washiriki wa mafunzo hayo walisema aina hiyo
ya uvuvi haijasaidia kuwakomboa kiuchumi kwa sababu ni lazima ifanywe na
watu wengi zaidi.
"Ukiangalia hali zao
wale wanaofanya uvuvi halali wa kutega wanaonekana kuwa na maisha bora
zaidi kuliko wale wanaovua kwa kutumia makokoro yanayouzwa kwa bei
kubwa," alisema Mbawala.
Katika kuwanusuru
samaki hao na wengine wanaotakiwa kuvuliwa kihalali mmoja wa washiriki
katika mafunzo hayo, Leonard Ndilwa alisema; "Zamani kulikuwa na
utaratibu wa wavuvi kuruhusiwa kuvua kwa siku zisizozidi 20 kila mwezi
na kuacha siku nyingine kumi kuwawezesha samaki kuzaliana na kukua."
Mshiriki mwingine
Hussein Magomba alisema, Serikali imeshindwa kukabiliana na wavuvi
wanaotumia makokoro na ndio maana uvuvi huo unaonasa samaki wadogo na
wakubwa bado unaendelea.
Wengine wakasema
hawawezi kuacha aina hiyo ya uvivu, labda serikali itakaposaidia
kuwasambazia nyavu halali za uvuvi kwa bei ndogo.
Mshiriki mwingine
Agripina Thomas alisema, shida kubwa ya wavuvi wa vijiji hivyo
kujiingiza katika shughuli ya uvuvi haramu ni kutoshiriki katika
shughuli nyingine za uzalishaji mali kama kilimo.
Mkurugenzi wa MMADEA,
Raphael Mtitu alisema uvuvi haramu unatumia zana zinazoharibu mazingira
na hivyo kuchangia mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema katika kukabiliana na mabadiliko hayo wavuvi wanapaswa kufanya shughuli zingine za kiuchumi kama kilimo na ufugaji.
0 comments:
Post a Comment