Home » » Washindi Redd’s Uni-Fashion Bash Iringa wapatikana

Washindi Redd’s Uni-Fashion Bash Iringa wapatikana


KUMEKUCHA: Washindi wanamitindo na wabunifu walio katika vyuo vikuu katika Mkoa wa Iringa walioshiriki shindano la ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’, lililofanyika mwishoni mwa wiki ndani ya Ukumbi wa Shooter’s mjini hapa, wamejulikana.

Katika shindano hilo wanamitindo waliofanikiwa kuibuka na ushindi ni Noel Ndale kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, aliyejipatia Sh 500,000 huku nafasi ya pili ikitwaliwa na Lillian Ramadhan pia kutoka Tumaini, aliyeondoka na kitita cha Sh 400,000.

John Mwakibete wa Chuo Kikuu cha Ruaha alipata nafasi ya tatu na kujishindia Sh 300,000 wakati Jonathan Justine pia kutoka Ruaha na Christina Mwakigonja wa Chuo Kikuu Mkwawa walishika nafasi ya nne na tano na kila mmoja kujipatia Sh 100,000.

Kwa upande wa wabunifu Esther Amas wa Ruaha alishinda na kutwaa Sh 700,000 akifuatiwa na Caroline Sumary wa Mkwawa aliyepata Sh 500,000 wakati Doreen Dustan wa Tumaini akikamata nafasi ya tatu na kupata Sh 300,000 huku nafasi ya nne na tano ikishikwa na Kwetukia Eunice wa Ruaha na noel Ndale wa Tumaini walioondoka na Sh 100,000 kila mmoja.

Tamasha hilo linalochochea vipaji ndani ya vyuo hivyo, awali lilifungua pazia ndani ya Mkoa wa Mwanza na Kilimanjaro na litahusisha pia vyuo vilivyopo Mkoa wa Dar es Salaam.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah alisema, wamefurahishwa mno na ushiriki wa wanafunzi ndani ya Iringa na wanaamini Dar es Salaam watakuwa wamejiandaa vya kutosha.

Fimbo alisema, wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu ya juu walio na mapenzi katika ubunifu na mitindo wanatarajiwa kushiriki shindano hilo, huku akiamini kutakuwa na upinzani mkali zaidi ya ule wa Mwanza, Kilimanjaro na Iringa.

Kinywaji cha Redd’s Original pia ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa