Na. Aron Msigwa- MAELEZO.
Wakati
maadhimisho ya Wiki ya Vijana kitaifa yakiingia siku ya tatu mkoani
Iringa Serikali imewahakikishia vijana kuwa itaendelea na mkakati wake
wa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ili waweze
kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha na kuondokana na
umasikini.
Akizungumza
na Vijana wanaoshiriki maadhimisho hayo mkoani Iringa Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Amos Makala amesema kuwa
serikali katika kuhakikisha inatimiza lengo hilo kwa kuanzia imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 6.1 katika bajeti ya mwaka 2013/2014 ili
kuwawezesha vijana kote nchini.
“Jambo
hili la kuwawezesha vijana tunalipa uzito mkubwa na kwa kuanzia katika
bajeti ya mwaka huu tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.1 kuwawezesha
vijana, ni mwanzo mzuri pamoja na kuwa tunahitaji kufanya zaidi”
amesema
Amefafanua
kuwa kiasi hicho cha fedha kitatolewa kwa vijana walioamua
kujishughulisha na wenye mawazo ya kujikwamua kiuchumi na kuwataka
vijana kote nchini kutumia fursa ya mikopo wanayopata kuitumia katika
kufanya shughuli za maendeleo.
“Nawaomba
vijana muepuke kutumia fedha hizo katika anasa na mambo mengine
yasiyokusudiwa yanayowafanya mjikute mmeingia katika matatizo ya
madeni na kuendelea kuwa maskini” amefafanua
Hata
hivyo amesema serikali kwa kuliona jambo hilo imeandaa mpango wa
kuwapatia elimu vijana ili waweze kuzitumia ipasavyo fursa za maendeleo
zilizopo na waweze kujiandaa kunufaika na kiasi hicho cha fedha
zilizotengwa pia inafanya jitihada za kuboresha vyuo vya vijana pamoja
na kuongeza idadi ya walimu wa vyuo hivyo.
“Nataka
niwahakikishie kuwa serikali inaendelea kuviboresha vyuo vyetu vya
ndani ikiwa ni pamoja na kushirikiana na nchi marafiki ambapo kwa
kushirikiana na Afrika ya Kusini tunaandaa utaratibu wa kupeleka walimu
wetu ili waweze kusoma huko na kuja kufundisha vijana katika vyuo vyetu”
amesema.
Mh.
Makala ameongeza kuwa tayari serikali katika kushughulikia tatizo la
ajira hasa kwa vijana wanaohitimu masomo ya elimu ya juu kwa kuzungumza
na baadhi ya taasisi za fedha zikiwemo benki za NMB, EXIM Bank na CRDB
ili ziweze kutoa mikopo kwa vijana hao kwa dhamana ya vyeti vyao na
kubainisha kuwa tayari baadhi ya benki zimekwisha anza zoezi la
kuwakopesha vijana kwa kutumia dhamana ya vyeti vyao.
Aidha
kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Vijana kitaifa amesema kuwa inatokana na
uamuzi waserikali uliofanyika mwaka 1999 mjini Dodoma wa kuhakikisha
kuwa kila mwaka vijana wanapata fursa ya kujumuika pamoja katika
maadhimisho hayo.
Aidha
amewashukuru viongozi wa mkoa wa Iringa kwa maandalizi mazuri
waliyoyafanya ya kwa kushirikiana na viongozi wa Wizara ya Habari Vijana
, Utamaduni na Michezo kuhakikisha kuwa shughuli za Wiki ya Vijana na
kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru tarehe 14/10/2013 zinafanikiwa kwa
kiwango kikubwa.
“Sisi
kama viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
tunawashukuru sana viongozi wa Iringa kwa ushirikiano mlioutoa katika
kufanikisha shughuli hizi za Wiki ya Vijana kitaifa, na ni matumaini
yetu kuwa tarehe 14 mwezi huu wananchi wengi zaidi watajitokeza katika
kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2013” amesema Mh. Makala.
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi amesema
kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuwafanya vijana kujitambua na
kuwakumbusha kuzitumia fursa za kimaendeleo zilizo katika maeneo yao
kujiletea maendeleo.
Amesema
katika maadhimisho ya mwaka huu licha ya kuwepo kwa maonyesho ya bidhaa
mbalimbali zilizotengenezwa na vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini
vijana watapata fursa ya kujadili mada mbalimbali katika midahalo
ikiwemo mada ya kuujua mkoa wa Iringa na fursa za kimaendeleo na ajira
zilizopo katika mkoa wa Iringa, pia huduma za hifadhi ya jamiii na
maendeleo ya vijana,nafasi ya vijana wa Tanzania katika kutunza amani na
upimaji wa hiari wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa mkoa wa
Iringa utaendelea kutoa msukumo kwa vijana ili waweze kujiletea
maendeleo kutokana na fursa zilizopo ndani ya mkoa huo.
Ameongeza
kuwa mkoa huo kwa muda mrefu umekuwa na jukumu la kuwaandaa vijana
kuwa watu wanaojitegemea, kuwa viongozi na watoa maamuzi sahihi,
wajasiriamali na wazazi wanaowajibika na kuongeza kuwa serikali ya mkoa
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kutoa elimu kwa vijana
kuhusu uzazi salama, ujasiriamali na kujikinga dhidi ya maambukizi ya
Ukimwi.
Dkt.
Ishengoma ameeleza kuwa mkoa wa Iringa umeanzisha mfuko wa kuwawezesha
vijana kwa kuwapatia mikopo na mitaji ya kuendesha miradi midogo midogo
ya kiuchumi na kuondoa tatizo za utegemezi na tayari vikundi vipatavyo
70 katika halimashauri za mkoa wa Iringa katika mwaka 2012/2013
vimepatiwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 116.
0 comments:
Post a Comment