KITUO cha kisasa cha Iringa Football for Hope
Centre kilichoko chini ya Shirika la Vijana, Walemavu na Watoto (IDYDC), la
mkoani hapa na kufadhiliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA),
kimezinduliwa rasmi na mbio za Mwenge.
Akisoma risala kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge, Lige
Masanja, alisema kituo hicho kina lengo la kukuza vipaji vya mpira na kutoa
elimu na ushauri nasaha kwa vijana.
Alisema hadi kukamilika kwake, kimegharimu sh
milioni 275 zilizotokana na ufadhili wa FIFA.
Naye Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ally
Simai, aliishukuru FIFA kwa msaada wa kituo hicho na kuwataka vijana kutambua
kuwa michezo ndiyo njia pekee ya kuwaunganisha katika kuleta amani na upendo
katika jamii.
Simai alisema kupitia michezo watu wengi wameweza
kuondokana na chuki, hivyo ni jukumu la kila mmoja kupenda michezo ambayo ni
yenye nafasi kubwa ya kutatua tatizo la ajira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile
Hosia, alilipongeza Shirika la IDYDC kwa kukamilisha mradi huo na kitendo hicho
kitakuza soka ya vijana kwa Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla na kuwataka
kutumia ipasavyo kituo hicho katika kufanikisha kukuza vipaji vya soka.
Alisema kwa kufanikisha kituo hicho, utakuwa mwanzo
wa FIFA kutoa fedha zaidi kwa ajili ya miradi kama hiyo nchini na kuitaka
serikali iongeze kasi katika ujenzi wa viwanja bora kwa lengo la kukuza michezo
nchini.
Naye Mkurugenzi wa IDYDC, Johnnie Nkoma, alisema
lengo la kituo ni kuwafikia watoto 8,000 lakini kitaanza kuwahudumia 200 kwa
sasa na kuwataka watoto wajitokeze kupata nafasi ya kujifunza michezo
mbalimbali.
Nkoma alisema kituo hicho kitakuwa kinatumika usiku
na mchana, kwani wanafunzi na watoto watakuwa wakipata mafunzo nyakati za jioni
wakati vijana na watoto wa mitaani watakitumia usiku kwa ajili ya mazoezi ya
kukuza vipaji vyao.
“ Katika kituo hiki vijana watakuwa wanapata
mafunzo ya afya ya uzazi na ugonjwa wa ukimwi, pia watapata nafasi ya kujua
afya zao kwa kupima ukimwi bure hapa hapa kituoni, kutoa ujuzi wa mpira wa
miguu na kutoa elimu ya kuimarisha uwezo wa vijana kuondokana na matumizi ya
madawa,” alisema Nkoma.
Alizitaja huduma zitakazokuwapo katika kituo hicho
kuwa ni ukumbi wa mikutano, maktaba, huduma ya mtandao wa ‘internet’, ushauri
nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment