Home » » WAKULIMA WAONDOLEWA HOFU MBOLEA YA MINJINGU

WAKULIMA WAONDOLEWA HOFU MBOLEA YA MINJINGU

na Amana Nyembo, Iringa
WAKULIMA mkoani Iringa wameondolewa wasiwasi wa kutumia mbolea ya Minjingu itakayokuwepo kwenye pembejeo za ruzuku msimu ujao kwa kuelezwa kuwa imeongezwa virutubisho, hivyo haina madhara kwa matumizi.
Awali wakulima walikuwa na hofu ya kutumia mbolea hiyo kutokama na mbolea hiyo iliyokuwa imegawiwa na serikali, kusababisha mavuno hafifu.
Akizungumza na wakulima hao hivi karibuni kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Mbigili na Lulanzi mbele ya wanahabari waliokuwa ziarani mkoani Iringa kwa ufadhili wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Ofisa Mazao na Pembejeo Wilaya ya Kilolo, Watson Matamwa, alisema Minjigu ni mbolea ya vumbi ni nzuri katika kilimo.
Alisema msimu uliopita mbolea hiyo ililetwa mapema bila maelekezo yoyote, lakini kwa sasa imefanyiwa kazi na wale walioitumia msimu uliopita na kupata mavuno kidogo msimu ujayo watapata mavuno mengi kutokana na mbolea, hivyo kudumu muda mrefu ardhini.
“Minjingu ni mbolea inayoweza kupambana na tindikali, haiharibu udongo, ni mbolea ya asili na ukiweka shambani mavuno yako yataendelea kuwa mazuri kwa miaka miwili hadi mitatu,” alifafanua Matamwa na kusema sasa imeongezwa virutubisho.
Awali akizungumzia mbolea hiyo, mkulima Yeteri Kiongosi kutoka Kijiji cha Lulanzi alisema mbolea hiyo walipoitumia haitoa tija yeyote katika kilimo cha mahindi.
Mpagama alisema: “Baada ya kupata mavuno kidogo, tulifanya majaribio katika mazao yote tukaona Minjingu inafaa katika zao la tumbaku na pareto.”
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa