na Francis Godwin, Iringa
KASHFA ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa kutuhumiwa kudanganya umri wao wa kuzaliwa, imechukua sura mpya baada ya idadi kubwa ya vijana waliojaza fomu za kuomba nafasi mbalimbali katika umoja huo kukimbia kikao cha usaili.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Salim Abri Asas na Katibu wa Mkoa, Emmanuel Mteming'ombe kupigilia msumari kwa kutaka haki itendeke katika kuchuja majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali bila upendeleo wowote na wale waliochakachua miaka kuwajibishwa.
Hiyo inakuja baada ya gazeti hili kuibua siri nzito kuwa karibu robo tatu ya vijana wamedanganya umri kwa kujaza uongo, wengi wao wakirudisha nyuma miaka yao ya kuzaliwa ili iweze kuendena na kanuni ya UVCCM inayomtaka mgombea kuanzia miaka 14-30.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili juzi katika ukumbi wa CCM Mkoa wakati wa kikao cha kupendekeza majina ya wagombea, ambapo taarifa walizojaza katika fomu zao za kuomba nafasi mbalimbali uhakikiwa, sehemu kubwa ya wanachama waliojaza fomu walishindwa kutokea.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ambazo zimethibitishwa na baadhi ya wanachama zilidai kuwa walioshindwa kutokea katika kikao hicho ni baadhi ya wale wanaodaiwa kufanya uchakachuaji wa umri katika zoezi la ujazaji wa fomu.
Mmoja kati ya wanachama hao alisema taarifa ya Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa iliyotolewa katika moja ya vyombo vya habari kuhusiana na hatua ambazo zitachukuliwa kwa wale wote waliodanganya miaka yao ya kuzaliwa, ndizo zilizowatisha na kuamua kukimbia zoezi hilo la usaili.
“Kweli hatua ya katibu kutoa tamko hilo dhidi ya waliodanganya umri ndiyo imesababisha kuwepo kwa idadi ndogo ya wagombea hao kufika katika kikao hicho na kufanya wawepo 15 kati ya wanachama zaidi ya 44 waliojaza fomu za kuomba nafasi mbalimbali,” alisema.
Katibu wa UVCCM mkoa wa Iringa Rhoda George alithibitisha kutofika kwa baadhi ya wagombea, akisema hakuna taarifa zao.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa suala la umri halitakuwa na msalie mtume na kuwa UVCCM Mkoa wa Iringa itatekeleza maagizo ya katibu mkuu wa UVCCM taifa ambayo tayari yametolewa kwa wale waliodanganya miaka ya kuzaliwa kuwajibishwa kisheria.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment