Home » » RC: WANAHABARI SAIDIENI SENSA

RC: WANAHABARI SAIDIENI SENSA

na Francis Godwin, 
Iringa MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amewataka wanahabari kulisaidia taifa katika zoezi la sensa ya watu na makazi kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi hilo.
Rai hiyo ilitolewa jana katika ukumbi wa Ruco mjini hapa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Mkoa wa Lindi na Mtwara.
Alisema kuwa, zoezi hilo la sensa ya watu na mkazi, lina umuhimu mkubwa kwa taifa kwani itaiwezesha Serikali kupanga bajeti kulingana na mahitaji sahihi ya wananchi wake, hivyo kuwataka wanahabari hao kusaidia kutoa elimu kwa umma.
Alisema, ni wajibu kwa wanahabari kuelimishwa zaidi juu ya zoezi hilo litakavyofanyika kama njia ya kuwezesha taifa kufanikisha zoezi hilo.
Alisema, vyombo vya habari ni miongoni mwa wadau wakubwa ambavyo vinategemea zaidi takwimu katika kufikisha ujumbe kwa taifa hivyo ili zoezi hilo liweze kufanikiwa lazima kuwepo na ushirikiano mkubwa kutoka kwa vyombo hivyo vya habari.
Dk. Ishengoma alisema kwa vile zimesalia siku 13 kabla ya zoezi hilo la sensa, ni matumaini ya serikali kuona siku zilizobaki zinatumika vema katika kufikisha taarifa kwa wananchi.
Alisema, sensa ya watu na makazi ni zoezi ambalo limekuwa likifanyika kila baada ya miaka 10 hivyo lazima umma kujulishwa ili kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alishauri wakuu wa kaya kuweka kumbukumbu sahihi ambazo zitawezeshwa makalani wa sensa kupata taarifa zilizo sahihi katika kufanikisha zoezi hilo.
Aidha, alisema kuwa ni marufuku kwa makalani wa sensa nchini, kuomba posho kwa wananchi wanaokwenda kuwahesabu, wala makalani hao kuongeza idadi ya maswali ambayo hayamo katika orodha ya maswali yaliyomo katika dodoso fupi ama Dodoso refu.
Pia, aliwataka wale wote ambao wamepewa nafasi ya kufanya kazi hiyo ya sensa, kutotoa siri ya taarifa za wale ambao wamehesabiwa.
Katika semina hiyo inayomalizika leo, wanahabari walioshiriki ni kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Njombe na wenyeji Iringa
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa