Home » » PROF. MSOLLA ALALAMIKIA UTARATIBU WA WIZARA YA KILIMO

PROF. MSOLLA ALALAMIKIA UTARATIBU WA WIZARA YA KILIMO


Mwandishi wetu, Iringa Yetu

MOJA ya sababu inayokwamisha sekta ya kilimo na mifugo ni utaratibu wa kuzichanganya idara hizo na kuwa katika Wizara moja, jambo linalochangia uhaba wa watumishi na hivyo kushindwa kufanikisha
kaulimbiu za serikali ikiwemo Kilimo Kwanza.

Hayo yalibainishwa na Profesa Peter Msolla wakati wa mahafali ya kwanza ya wahitimu 44 wa chuo cha kilimo cha Mtakatifu Maria Goretti, kilichopo Ilula/Image, katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, ambaye ni mbunge wa jimbo la Kilolo.

Amesema kuzichanganya sekta hizo mbili katika Wizara moja ni sababu ya kilimo kushindwa kufanikiwa kwa kiwango kikubwa, kwani Kilimo na Mifugo ilitakiwa ziwe wizara mbili tofauti zinazojitegemea ili kufanya kazi kwa ufanisi, ikiwa pamoja na kuwepo kwa wataalamu  waliobobea kwa fani moja moja.


Amesema kilimo cha Tanzania kinakuwa duni kutokana na mkanganyiko huo, ikiwa pamoja na wakulima wake kuendeleleza matumizi ya zana duni, ikiwemo jembe la mkono, na kuwa hali hiyo inatokana na uwepo wa
asilimia 10 pekee inayotumia zana bora za kilimo za kisasa (Matrekta) huku asilimia 67 ya wakulima wakitumia jembe la mkono, na asilimia 22 wakitumia wanyamakazi.


Aidha amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwa mabarozi wema kutoka katika chuo hicho, ikiwa pamoja na kuwashauri wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kufanikisha kilimo, na kuwa washauri wema wa wakulima ili kukuza sekta hiyo.

Aliwahimiza wahitimi hao kutobweteka na elimu hiyo, na kuwataka wajiendeleze zaidi ili kuingia katika ushindani wa soko la ajira ambao mtaji wa uhakika ni elimu pekee, na kuachana na fikra za kuajiriwa na badala yake wabuni shughuli za kujiajiri wao wenyewe.
Hata hivyo wahitimu walilalamikia changamoto zinazokwamisha mafunzo katika chuo cha Mtakatifu Maria Goretti ikiwa pamoja na kutokuwepo kwa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, zikiwemo Kompyuta, Maabara,  uhaba wa wakufunzi na tatizo la usafiri.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa