Home » » MADIWANI WAMLAUMU DC KUKIUKA TARATIBU

MADIWANI WAMLAUMU DC KUKIUKA TARATIBU


na Mwandishi wetu, Mufindi
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi limemlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo kwa kukiuka taratibu za uendeshaji wa Mfuko wa Elimu na kusababisha mwenendo wa matumizi mabaya ya mfuko huo.
Imeelezwa mfuko wa elimu katika wilaya hiyo umekuwa ukiendeshwa kinyume cha sheria ndogo za halmashauri na kuonekana si mfuko wa umma, bali ni wa mtu binafsi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu kuunda kamati ya kusimamia mfuko huo bila kulishirikisha baraza la madiwani kama taratibu zinavyoelekeza.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Peter Tweve, alisema kutokana na uchunguzi wa baraza lao kupitia kamati ndogo ya uchunguzi, ilibaini uendeshwaji wa mfuko huo haukuwa mzuri.
“Sisi kama Baraza tuliamua kufanya uchunguzi kwenye mfuko wa elimu kupitia kamati yetu na ilibaini kuwa utaratibu uliokuwa ukitumika kukusanya mapato na matumizi ya mfuko kutokuwa sahihi kwa kuwa sheria ya Bodi ya Mfuko wa Elimu ilishakuwa imetangazwa kwenye tangazo la Serikali namba 482 la Desemba 26 mwaka 2008, lakini kamati ya mfuko huo haikutekeleza taratibu husika,” alisema Tweve.
Alisema kamati yake ilijiridhisha na kuona kuwa utaratibu wa matumizi ya mapato ya mfuko wa elimu hayakuwa na utaratibu wa kueleweka kwa kuwa maamuzi ya matumizi hayakuwa ya vikao vya kamati ya mfuko, bali yaliamriwa na mkuu wa wilaya kama mwenyekiti kwa kutoa maelekezo ya matumizi.
Alisema kutokana na uchunguzi huo, kamati yake ilibaini mapato katika mfuko wa elimu kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 yalikuwa sh. 278,287,843 lakini katika matumizi kulionekana kuwa na utofauti.
Alisema Baraza la madiwani la Januari 11 mwaka 2012 lilipokea taarifa kuwa hadi kufikia Desemba 2011 mfuko wa elimu ulikuwa umetumia kiasi cha sh 180,872,124.65, lakini kamati ilibaini hadi kufikia Desemba 2011 mfuko huo ulikuwa umetumia sh.258,260,870 na kuwa na tofauti ya sh 77,388,746.35 ambayo ni matumizi zaidi ya yale yaliyoripotiwa.
Aliongeza baada ya kujiridhisha kamati yake ilitembelea mahali fedha za mfuko huo zilikoelekezwa, lakini zilibaini mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na fedha hizo kutumika kujenga majengo ya shule chini ya kiwango.
Tweve alisema kutokana na kubaini mapungufu hayo, kamati yake ilitoa mapendekezo ya kuitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkrugenzi kufanya kazi zao kama taratibu za halmashauri zinavyowaongoza.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu, alikanusha madai hayo na kusema fedha zilizokuwa zikikusanywa kwa ajili ya mfuko huo zilikuwa juhudi zake binafsi na hivyo alikuwa akitekeleza hilo kama mkuu wa wilaya na kwamba baada ya makusanyo zilikuwa zikipelekwa katika ofisi ya mkurugenzi kwa ajili ya kupangiwa matumizi yaliyokusudiwa.
“Fedha hizi zilikuwa zikipatikana kwa juhudi zangu binafsi kwa kuwaomba wadau na marafiki wa elimu na hivyo baada ya makusanyo zilikuwa zikiwasilishwa kwa mkurugenzi kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.
Hivyo mimi kama mkuu wa wilaya nilikuwa natimiza wajibu wangu kwa kushirikiana na wadau kwa ajili ya kuihudumia jamii,” alisema Kalalu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa