Home » » Neno La Leo: Kwenda Kupiga Kura Ni Kwenda Kuchagua..‏

Neno La Leo: Kwenda Kupiga Kura Ni Kwenda Kuchagua..‏


Ndugu zangu,
Leo ni siku ya kupiga kura kwenye Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Huu ni Uchaguzi Muhimu sana katika nchi. Uchaguzi huu ndio MSINGI wa siasa kubwa za Kitaifa.
Siasa ya nchi inaanzia kwenye Mtaa, Kijiji na Kitongoji. Na hakika, siku ya leo ilipaswa uwe ni uchaguzi pia kwa ngazi ya Manispaa na Halmshauri, kwa maana ya kuwachagua Madiwani.
Inahusu Serikali za Mitaa ( Local Goverment). Nimepata kuandika, kuwa Mahtama Ghandhi alipata kusema, kuwa ukitaka kuujua moyo wa nchi, nenda vijijini.
Katika nchi zetu hizi, uchaguzi wa leo ni kipimo cha Uchaguzi Mkuu ujao. Chama ama kambi itakayofaulu kupata asilimia 80 ya viti vyote vinavyogombaniwa, basi, naweza kuandika hapa, Kuwa ni ndio chama au kambi itakayounda Serikali baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani.
Na kama kwenda kupiga kura ni kwenda kuchagua swali ni je, wapiga kura wanajua wanachokwenda kuchagua? Jibu, yumkini kuna wapiga kura wenye kwenda kuchagua sura na majina ya watu, lakini, kwa wengi waliohamasika au kuhamasishwa kujiandikisha, leo Jumapili wanakwenda kuchagua wanachokijua na kukiamini.
Na siasa ni itikadi, na kwenye itikadi, kama nilivyoandika huko nyuma, kuwa kuna KULIA na KUSHOTO. Ni imani. Hivyo, kuwa na msimamo kisiasa ina maana ya kusimama ama Kulia, au Kushoto. Kushoto ni wenye mrengo wa Kijamaa na Kujitegemea na kujali zaidi maslahi ya walio wengi. Kushoto ni Mrengo wenye kusimamia katika Haki na Usawa kwenye jamii. Kulia ni upande wa Mabwanyenye ama Mabepari. Ni wenye kuamini zaidi katika Mtaji na kukuza mtaji, bila kujali maslahi ya wengi. Na walio kwenye upande huo, wanaamini, kuwa Kutokuwepo kwa Usawa kwenye jamii ni jambo lisiloepukika.
Na kuna Katikati ya kiitikadi, kwamba kuna waliosimama kati. Lakini, aliyesimama kati anapo anapoegemea. Hivyo, kuna waliosimama kati wakiegemea Kushoto na wengine wakiegemea Kulia. Nao waweza kuwa viongozi bora, kama mpiga kura atafanya maamuzi yake.
Leo tunakwenda kuwachagua viongozi wetu kwenye Mitaa yetu, Vijiji na Vitongoji. Na kuna kisa cha mume aliyegombea nafasi ya uongozi. Alikwenda kituo cha kupigia kura na mkewe. Kura zilipohesabiwa aliambulia kura moja, ya kwake mwenyewe. Nyumbani akamuulizia mkewe; " Hivi mke wangu hata wewe hukunipigia kura?"
Mkewe akajibu: " Mume wangu, tulikwenda kupiga kura kumchagua Kiongozi Bora, na kama ingelikuwa kumchagua Mume Bora, kura yangu ingeangukia kwako!"
Naam, e twendeni tukapige kura kuwachagua viongozi bora, nao watokane na itikadi bora wenye kuzisimamia.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa