Home » » MILIONI 400 ZA OFISI YA RAIS – TAMISEMI KUJENGA NA KUKARABATI KITUO CHA AFYA MALANGALI HALMASHAURI YA MUFINDI

MILIONI 400 ZA OFISI YA RAIS – TAMISEMI KUJENGA NA KUKARABATI KITUO CHA AFYA MALANGALI HALMASHAURI YA MUFINDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mufindi itatumia jumla ya shilingi Milioni Mianne (400) kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa kituo cha Afya Malangali, kilichopo kata ya Malangali Halmashauri ya Wilayani Mufindi, ikiwa ni mkakati wa Serikali kuimarisha sekta muhimu ya Afya hususani Afya ya Mama na Mtoto.

Ujenzi na ukarabati wa kituo hiki cha Afya, unaotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa, unafanyika baada ya Ofisi ya Rais – Tamisemi, kutoa kiasi cha Shilingi Milioni mianne (400) kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya kituo hicho ili kiweze kukidhi haja ya kutoa huduma bora za Afya kwa zaidi ya Wananchi elfu arobaini na nane (48,000) wa Tarafa ya Malangali watakao pewa rufaa kutoka kwenye Zahanati za Vijiji.

Matumizi ya kiasi hicho cha fedha, ni pamoja na kujenga jengo la kisasa la Maabara, Nyumba ya Mganga, kukamilisha ujenzi unaoendelea wa chumba cha upasuaji sanjari na kufanya ukarabati mkubwa wa Wodi maalum ya wazazi / Mama na Mtoto.

Ujenzi na ukarabati wa kituo, utatekelezwa kwa mfumo wa (Force Account) ambapo, Halmashauri itatumia Mafundi wenyeji watakaothibitishwa kuwa na uwezo unaokubalika wa kutekeleza jukumu hili kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu, badala ya mtindo uliozoeleka wa kutumia Wakandarasi. Pia, ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji, imeunda Vikosi kazi vitatu (03) vikijumuisha Maofisa kutoka idara mbalimbali maalum kwa kuratibu na kusimamia mradi huu kwa kuzingatia wakati na ubora.

Aidha, kwa kuwa uboreshaji wa kituo hiki, utatekelezwa kwa mfumo wa (Force Account) kama ambavyo imefafanuliwa hapo juu, Mkurugenzi Mtendaji anawahamasisha wananchi wote wa Tarafa ya Malangali kujitolea nguvu kazi pindi itakapohitajika wakati wa utekelezaji wa mradi huu kwa ustawi wa Afya ya kila mkazi wa Tarafa ya Malangali na Halmashauri ya Mufindi kwa ujumla.

Imetolewa na,

Ndimmyake Mwakapiso,
Ofisa Habari na Mawasiliano Halmashauri ya (W) Mufindi.
Profesa Riziki Shemdoe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi.
 

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa