MEYA wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe na wafuasi wenzake watano wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani
mjini Iringa, kujibu mashitaka yanayohusishwa na vurugu za uchaguzi
mdogo wa udiwani Kata ya Kitwiru, Iringa mjini.
Wakati Meya huyo aliachiwa jana kwa dhamana na Mahakama ya Wilaya
Iringa, baada ya kusota rumande kwa siku tatu, Mahakama ya Hakimu Mkazi
Iringa iliwanyima dhamana wafuasi hao watano kwa kuwa kati ya makosa
matatu, wanayotuhumiwa kuyafanya kosa moja halidhaminiki.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Aristeck Mwinyikheri alisema Kimbe
aliyefikishwa mahakamani hapo kwa kesi Namba 189 ya mwaka 2017,
anashitakiwa kutishia kumuua mtu kwa bastola katika tukio la Novemba 26,
mwaka huu katika Kata ya Kitwiru mjini Iringa, wakati shughuli ya
uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo ikiendelea.
Mwinyikheri alisema Meya huyo alitenda kosa hilo kwa Alphonce
Muyinga, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM), kinyume na Kifungu Namba 89 (2) (a) cha Kanuni za Adhabu.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia alisema
shauri hilo litarudi tena mahakamani hapo Desemba 12, mwaka huu. Wakati
huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imewanyima dhamana Martha
Robert, Leonard Kulijira, Esau Bwire, Christopher Jevas na Samwel
Nyanda, wafuasi wa Chadema ambao kwa pamoja wameshitakiwa mahakamani
kupitia kesi namba 190 ya mwaka 2017 kwa makosa matatu.
Mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Richard Kasele , Mwendesha
Mashitaka wa Mahakama hiyo Chakila Felix alisema washitakiwa hao wafuasi
wa Chadema, wanatuhumiwa kujeruhi, kuteka na kufanya unyang’anyi kwa
kutumia nguvu.
Felix alisema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kumjeruhi Dick Frank na
kumnyang’anya simu yake ya mkononi. Mahakama hiyo imewarudisha rumande
washitakiwa hao baada ya kunyimwa dhamana kwa kuwa kosa la unyang’anyi
kwa kutumia nguvu, halina dhamana na shauri lao litarudi tena mahakamani
hapo Desemba 12, mwaka huu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment