Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Acp. Julius A. Mjengi
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi/ Mkoa-Iringa, Mhe. David Ngunyale.
- Muonekano wa jengo la Mahakama ya Iringa, ndani ya uwanja huo kuna Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya-Iringa ‘Judiciary Square’
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Acp. Deusdedit Kasindo
Anayeonekana
pichani ni Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Acp. Deusdedit
Kasindo na kulia ni Afisa Ustawi wa Jamii, Halmashauri ya Iringa, Bw.
Bw. Ismail Mambo, katika mahojiano.
Kiongozi wa Dini ya Kiislamu mkoani Iringa, Sheikh Shams Elmi Obsiye.
………………………………..
Na Mary Gwera, Mahakama
Hivi
karibuni nilibahatika kutembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Iringa, miongoni mwa maeneo ambayo nilivutiwa nayo kutaka kufahamu
zaidi katika Kanda hiyo aina gani ya kesi/mashauri yanayofunguliwa kwa
wingi .
Mahojiano
maalum na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mkoa-Iringa, Mhe. David
Ngunyale yanabainisha kuwa Kesi za Unyanyasi wa Kijinsia hususani za Vitendo vya Ubakaji zinaongoza
kufunguliwa kwa wingi katika Mahakama mkoani humo huku akitaja idadi
kuwa kwa mwaka 2016 jumla ya kesi 62 zilifunguliwa katika Mahakama hiyo.
“Matukio
ya Ubakaji katika Mkoa wa Iringa yanazidi kushika kasi, hii
inajidhihirisha kufuatia takwimu za kesi/mashauri yanayofunguliwa
Mahakamani mwaka hadi mwaka, mfano kwa mwaka huu pekee hadi kufikia Juni
jumla ya kesi 36 tayari zilifunguliwa hali hii inaonyesha kuwa hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka huu kutakuwa na kesi nyingi za namna hii,”
alieleza Mhe. Ngunyale.
Kufuatia
hali hii, Hakimu huyo Mkazi anaeleza kuwa Mahakama inazipa kipaumbele
zaidi kesi za namna hii kwa kuzisikiliza na kuzitolea maamuzi haraka
iwezekanavyo, hata hivyo Mhe. Ngunyale anakiri kuwa katika uendeshaji wa
kesi za namna hii wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na
baadhi ya walalamikaji kula njama na washitakiwa na matokeo yake kesi
inashindwa kuendelea, mashahidi kutotokea Mahakamani, baadhi kesi
kuhusisha ndugu ambao mara nyingine huelewana na hatimaye kusababisha
kesi kutoendelea.
Mhe.
Ngunyale anasema kwa mujibu wa sheria, endapo mtu hubainika kuwa
alishiriki katika kitendo cha ubakaji pasipo shaka Mahakama hutoa adhabu
ya kifungo cha miaka 30, viboko sita (6) na fidia kwa familia ya muathirika wa tukio hilo.
Aidha;
Hakimu huyo Mfawidhi amesifu ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na
Wadau wake mkoani humo ikiwa ni pamoja na Polisi, Wanasheria, Ustawi wa
Jamii katika uendeshaji wa kesi hizo.
Kwa
Upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), ACP. Deusdedit
Kasindo akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, ACP.
Julius A. Mjengi anakiri kuwa tatizo la kesi za Ubakaji kwa Mkoa huo lipo huku akitaja visababishi vya tatizo hilo kuwa ni pamoja na Ulevi wa kutumia Madawa ya Kulevya, pombe za kienyeji (ulanzi), Tamaa ya mapenzi hususani kwa watoto wa shule, kutelekezwa kwa watoto pamoja na umaskini.
Anafafanua
kuwa imani za kishirikina pia zinachangia ongezeko la kesi za aina hii
kwa kuwa katika imani za kishirikina Waganga wa kienyeji wamekuwa
wakiwadanganya watu kna kwa hali hii wanasababisha kwa kiasi kikubwa
kuongezeka kwa vitendo hivyo. Kwa mujibu wa takwimu, Mkuu huyo wa
Upelelezi alisema kuwa kwa mwaka 2016 zilipokelewa jumla ya kesi 259
kati ya kesi hizo 239 zilikuwa zinawahusu watoto akifafanua kuwa kubaka watoto ilikuwa ni kesi 203, kujaribu kubaka 11 na kulawiti zilikuwa kesi 25.
Aliongeza
kuwa kubakwa wanawake zilikuwa kesi 18, kujaribu kubaka ni kesi 2 na
hivyo kupelekea kuwa na idadi ya jumla ya kesi 259.
ACP Kasindo alisema kuwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hususani ubakaji wana umri kati ya miaka 2 hadi miaka 10.
Mkuu
huyo wa Upelelezi alidai kuwa kati ya kesi hizo 259 jumla ya kesi 163
zilifikishwa Mahakamani ambapo kati ya kesi hizo zilizofikishwa
Mahakamani jumla ya Watuhumiwa 41 walitiwa hatiani, kesi nyingine
zilizobaki zinaendelea kusikilizwa Mahakamani.
Akizungumzia juu
ya kesi walizopokea Polisi kwa mwaka huu, 2017 hadi kufikia mwezi Mei,
Mkuu huyo wa Upelelezi alisema wamepokea jumla ya kesi 139 ambapo kati
ya kesi hizo zinazowahusu watoto pekee ni jumla ya kesi 121.
“Kubaka
peke yake ni kesi 98, kujaribu kubaka ni kesi 7, wanawake zipo kesi 18,
kati ya hizi 17 ni kubaka na kujaribu kubaka na zilizopelekwa
Mahakamani ni kesi 105, na waliotiwa hatiani ni 12, walioachiliwa ni 45,
na zinazoendelea Mahakamani zipo 48 huku mafanikio yakiwa ni asilimia
10 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu,” alieleza ACP. Kasindo.
Aidha,
ACP. Kasindo alieleza kuwa kuna changamoto ya kesi nyingi zinazopelekwa
Mahakamani kukwama, huku akitoa sababu ya kusuasua kwa kesi hizo kuwa
ni pamoja na umri mdogo wa Wahanga unaosababisha kushindwa kujieleza kwa
ufasaha, Watuhumiwa wa makosa hayo kuwa ndugu mfano baba na mtoto,
mjomba na mpwa na kadhalika, baadhi ya ndugu kuanza kusuluhishana na
hatimaye kuelewana hali inayosababisha kesi kutoendelea.
Katika
jitihada za kuendelea kupambana na vitendo hivyo, Mkuu wa Upelelezi
mkoani humo anasema kuwa kuna mikakati kadhaa wameweka ili kudhibiti
vitendo hivyo, akitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha Vipindi
vya Redio, kuelimisha jamii, mikutano na wananchi, kufanya semina kwa
kushirikiana na NGOs pamoja na Ustawi wa Jamii kwa Viongozi ambao wapo
karibu na Wananchi, kushughulikia kwa haraka zaidi mashitaka ya aina
hiyo.
ACP.
Kasindo amekemea vikali vitendo hivyo vya ubakaji huku akisema vitendo
hivi vinavyofanywa ni kosa la jinai na dhambi kwa Mungu, hivyo kuwaasa
wananchi kuacha ulevi wa kupindukia pamoja na kuachana na imani za
kishirikina.
Katika
mwendelezo wa kutaka kujua vyombo mbalimbali katika mkoa wa Iringa
vinafanya nini katika kudhibiti na kutokomeza vitendo hivi, nilifanikiwa
pia kuonana na Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Bw. Ismail
Mambo ambaye anafafanua kwa undani kuhusu vitendo vya unyanyasaji na
ukatili dhidi ya watoto.
“Tunapozungumzia
ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto tunamaanisha kwamba ni vile
vitendo ambavyo vinamuathriri mtoto katika ukuaji wake hasa kiakili,
kimwili na kihisia,” alifafanua Bw. Mambo.
Anasema
kutokana na hilo unakuta watoto wanaofanyiwa vitendo vya ubakaji na
udhalilishaji ni wale waliopo chini ya umri wa miaka 18, Bw. Mambo
anasema kuwa vitendo hivyo wafanyiwavyo watoto ni pamoja na Ubakaji, Ulawiti, pamoja na Kutelekezwa na wazazi.
“Kuna
watoto wengi wanafungiwa majumbani bila msaada wowote wakati wazazi wao
wakiwa katika shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato, pia watoto
hutelekezwa kwa kukosa matunzo kutoka kwa wazazi kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo mimba zisizotarajiwa, ulemavu wa watoto, mimba za
utotoni,” alieleza Bw. Mambo.
Afisa
huyo anasema kutokana na tatizo hilo, Halmashauri imeweka mikakati
kadhaa ya kukabiliana/kudhibiti ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kamati za
mitaa za kuhudumia watoto waishio katika mazingira hatarishi, moja ya
kazi ya Kamati hizo za Mitaa ni kuibua vitendo vyote vinavyotokea katika
mitaa yao vinavyohusu ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto na
kuviripoti kwenye kamati ya Ulinzi na Usalama ya mtoto na kwa
kushirikiana na Kamati hiyo huenda moja kwa moja kuripoti Kituo cha
Polisi katika dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto la Polisi na hapo
hatua mbalimbali huchukuliwa kati ya Polisi na Ustawi wa Jamii ikiwemo
kuhakikisha kwamba mtoto mhanga anapata haki stahiki ikiwa ni pamoja na
kupata matibabu, kuusikilizwa na kupatiwa huduma za taratibu za kisheria
katika ngazi ya Mahakama.
Hata
hivyo Bw.Mambo anadokeza kuwa uelewa wa jamii katika suala zima la
malezi ya watoto umeongezeka kwa kiasi fulani, zamani watu walikuwa
hawatoi taarifa kutokana na kuwa na uelewa mdogo pamoja na uwoga.
“Katika
Sheria ya mtoto namba. 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 95 kifungu kidogo
cha kwanza (1) kinazungumzia wajibu wa kuripoti ukiukwaji wa haki za
mtoto,” alifafanua Bw. Mambo.
Anaendelea
kueleza Mikakati iliyopo Ustawi wa Jamii mkoani humu akitaja kuwa ni
pamoja na kutoa elimu ya malezi katika ngazi ya jamii, kuanzisha vikundi
kwa kila mtaa vinavyotoa elimu ya malezi kwa kila kaya na kusimamia
utekelezaji wake (kati ya kuhudumia watoto waishio katika mazingira
hatarishi, kutoa mafunzo kwa Wasaidizi wa Jamii (Para Social) wawili
wawili (2) kwa kila mtaa.
Anaongeza
kuwa; mkakati mwingine ni kufanya ufuatiliaji wa karibu wa Wataalamu na
Wanachama wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ngazi ya Halmashauri katika
kamati za watoto waishio katika mazingira hatarishi ngazi za mitaa na
kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya suala zima la ulinzi na usalama wa
mtoto.
Afisa
Ustawi huyo wa jamii alimalizia kwa kusema kuwa katika mitaa yote 192
ndani ya Manispaa ya Iringa imefikiwa katika mafunzo na kupewa mafunzo
na kuteua makundi ya ‘Para Socials’ na Wasaidizi wa Ustawi wa jamii.
Naye,
Sheikh Shams Elmi Obsiye, Katibu Mkuu- Taasisi ya DHI, NUREYN-
Islamic-Iringa naye alizungumzia juu ya tatizo hili na kukiri lipo kwani
tayari Viongozi wa dini wa Mkoa huo walishadokezwa na Mkuu wa Mkoa juu
ya uwepo wa tatizo hilo.
“Ni
kweli tatizo hili lipo mkoani kwetu, kwa upande wetu Viongozi wa Dini
ya Kiislamu tunajitahidi kuhamasisha jamii kupitia Madrasa za Watoto,
ambapo kwa sasa tuna jumla ya Madrasa 25, na katika Madrassa zetu
miongoni mwa mambo tunayowafunza watoto ni pamoja na kuwafahamisha
kuhusu vitendo vinavyoashiria ubakaji mfano kununuliwa pipi, kupakatwa, kuitwa mchumba nk, madrasa zote zinafundisha hivyo,” alieleza Sheikh Obsiye.
Aliongeza
kuwa katika Redio yao iitwayo Kibla Ten Fm iliyopo mkoani Iringa, huwa
wana kipindi kinachohusu masuala ya Udhalilishaji wa Kijinsia ambapo
hutoa elimu ili wananchi waweze kujua vitendo hivyo ni kosa la jinai na
havimpendezi Mwenyezi Mungu.
“Mbali
na vitendo vya ubakaji ambavyo vinaripotiwa katika misikiti yenu, yapo
pia matendo mengine ya unyanyasaji wa Kijinsia kama baadhi ya wanaume
kuwapiga wake zao na kadhalika,” alibainisha Sheikh Obsiye.
Alisema
kuwa kwa mwezi wanapokea malalamiko mbalimbali zaidi ya 30, hata hivyo
Sheikh huyo amevitaka vyombo husika kutoa elimu zaidi kwa Viongozi wa
Dini ili kuwapa mbinu zaidi ya jinsi ya kushughulikia kesi za ubakaji na
nyingine zinazohusiana na unyanyasaji wa kijinsia.
Aidha
Sheikh huyo pia alivitaka Vikundi vingine vya Jamii kushiriki katika
kupambana na vitendo hivi, mfano Makundi ya akina mama wanaweza pia
kushiriki kutoa elimu kwa watoto juu ya viashiria vya vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia na umuhimu wa kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo
kwa vyombo husika vya sheria.
Vitendo
vya Ubakaji na Udhalilishaji wa Kinjisia, vimekuwa vikishika kasi kila
uchwao hali ambayo inapelekea wasiwasi na hali ya kutoaminiana miongoni
mwa wanajamii, aidha; vitendo hivi ambavyo vinasababishwa na imani za
kishirikina, tamaa, Utandawazi na masuala mengineyo kama ilivyoelezwa na
Wataalam katika makala hii.
Hivyo
kuna umuhimu mkubwa kwa Wazazi, Walimu, Viongozi wa Dini na kila mmoja
kwa nafasi yake kushiriki kwa namna moja au nyingine katika kuelimisha
na kutahadharisha makundi mbalimbali katika jamii kama watoto juu ya
viashiria vya vitendo hivi na umuhimu wa kutoa taarifa kwa vyombo husika
ikiwa ni pamoja na Ofisi za Serikali za Mitaa, Polisi katika Dawati la
Jinsia, Ustawi wa Jamii, Makanisani, Misikitini n.k
Vilevile
Wanaharakati wa Masuala ya Kijinsia, Ustawi wa Jamii na vyombo
vinginevyo vinavyojihusisha na kupigania haki za binadamu, kuangalia
uwezekano wa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa njia ya semina, vipindi
vya redio na runinga na njia nyinginezo ili kuwafikia wananchi wengi ili
vitendo hivi viweze kutokomea kabisa.
0 comments:
Post a Comment