Na: Lilian Lundo – MAELEZO
21/06/2016
Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imesema kuwa sera yake ya kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa kifua kikuu,
ukimwi, mama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano
inaendelea.
Hayo
yamesemwa leo, mjini Dodoma na waziri wa wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu
alipokuwa akitolea ufafanuzi wa swali la Mbunge wa Chalinze Mhe.
Ridhiwani kikwete juu ya taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa
utoaji wa dawa bure kwa makundi hayo ya watu umesitishwa na wanatakiwa
kulipia.
“Hakuna
mabadiliko yoyote katika sera ya kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa
ukimwi, kifua kikuu, mama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka
mitano, aidha nitaitaka hospitali ya Taifa ya Muhimbili inipatie maelezo
juu ya taarifa hizo,” alisisitiza, Mhe. Ummy.
Wakati
huo huo, naibu waziri wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla
amesema kuwa wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara ya Biashara, Viwanda
na Uwekezaji wanaandaa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa dawa nchini
ili angalau kukidhi asilimia 60 ya mahitaji katika kipindi cha miaka
mitano ijayo.
Aidha
wizara hiyo pia iko katika mikakati ya kuunda chombo cha kusimamia
gharama na bei zinazotozwa na vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa
pamoja na bei za dawa na vifaa tiba ili kuthibiti uongezaji holela wa
bei za dawa na vifaa tiba.
0 comments:
Post a Comment