Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
Agizo la serikali la kutoa elimu bure kuanzia shule
za msingi hadi kidato cha nne, limeanza kuonyesha matunda kwa baadhi ya
shule kuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi mkoani Iringa.
Hayo yamebainika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza,
juzi kutembelea na kukagua utekelezaji wa agizo hilo na changamoto
zake. Katika ziara hiyo, alibaini ongezeko hilo limesababisha upungufu
wa madarasa na madawati.
Akiwa katika shule za sekondari Kiwere, Kidamali na Kalenga,
Masenza aliarifiwa kuwapo na mwitikio mzuri wa wanafunzi kuripoti
shuleni huku wale walioacha kutokana na kukosa, ada wakiomba kurejea.
Sixtus Kanyama, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kidamali, alisema katika
shule yake wameongezeka zaidi ya wanafunzi 100, hatua ambayo
imesababisha kukaa wawili wawili.
Naye Blandina Nkondola, mkuu wa shule ya sekondari Kiwere, alisema
fedha zilizotolewa na serikali kwa kila mwezi, hazitoshelezi mahitaji
halisi ya msingi katika uendeshaji wa shule.
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa hakusita kutoa makucha yake kwa
shule ambazo wanafunzi hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza hadi sasa.
Aliagiza watendaji wa kata wasioweza kutekeleza wajibu wao wajifikirie
kama wanafaa kuendelea kuwamo katika nafasi zao.
Alisema kila mtendaji wa kijiji, atoe taarifa kwenye ofisi yake kwa
kutoa idadi ya watoto katika kijiji chake ambao hawajaripoti shuleni na
kupeleka taarifa kwa mtendaji wa kata.
Pia alitoa mwezi mmoja kwa shule ya Kidamali kukamilisha maabara
kama agizo la serikali linavyotaka, huku akielekeza shule zote ziwe
zimetatua tatizo la madawati ifikapo Mei, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, na
Mkurugenzi wake, Pudenciana Kisaka, walisema changamoto hizo zimeanza
kutatuliwa kwa kuanza kutengeneza madawati na kukamilisha ujenzi wa
maabara.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment