Home » » SAKATA LA VYAMA KUWA NA ULINZI BINAFSI ,UVCCM TAIFA YASEMA HAKUNA KIKUNDI CHA ULINZI CCM ,ILA IGP MANGU AWABANE CHADEMA NA CUF

SAKATA LA VYAMA KUWA NA ULINZI BINAFSI ,UVCCM TAIFA YASEMA HAKUNA KIKUNDI CHA ULINZI CCM ,ILA IGP MANGU AWABANE CHADEMA NA CUF

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

katibu  mkuu wa UVCCM Taifa  Bw  Sixtus Mapunda
Bw Mapunda  akizungunza na wanahabari mkoa wa Iringa
Katibu wa UVCCM mkoa  wa Iringa  Mwampasha kushoto akiwa na kiongozi wa UVCCM Taifa
Wanahabari  mkoa wa Iringa  wakimsikiliza katibu mkuu wa UVCCM Taifa  Bw  Sixtus Mapunda alipozungumza na  wanahabari hao
Na MatukiodaimaBlog

ZIKIWA  zimepita  siku  kadhaa toka mkuu  wa  polisi nchini (IGP), Ernest Mangu kupiga marufuku vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa ambavyo vina muonekano na muundo wa vyombo vya usalama kwa madai  ni  kinyume cha katiba na sheria ya nchi , umoja  wa  vijana  wa chama  cha mapinduzi (UVCCM) Taifa umejibu mapigo kuwa CCM hakuna vikundi  vya ulinzi kama chama  cha  demokrasia na maendeleo (chadema) na chama  cha  wananchi (CUF)

Katibu  wa UVCCM Taifa Sixtus Mapunda aliyasema hayo leo wakati wa  kikao  chake na  wanahabari mkoa  wa Iringa   kuwa  CCM inautaratibu  wa  kuwaandaa  vijana  kuwa  wazalendo na nchi  ya  na  kuwa mafunzo hayo  huanzia  ngazi ya chipukizi ambao kazi yao  kubwa ni  kuwavisha skafu viongozi  mbali mbali na  sio  kuwafundisha mafunzo ya kijeshi kama  ilivyo kwa upinzani hasa CUF na Chadema ambao juzi vijana  wake  wawili  wamekamatwa  Mbeya  wakiwa na dhana hatari za  kufundishia  mafunzo ya uharifu vijana  wao.


Alisema  kuwa  CUF  wana   ulinzi  wao kupitia
Blue Brigade huku Chadema wana kikundi chao  cha ulinzi cha  vijana ambacho ni
Red Brigade ila  baada ya vyama  hivyo  vya  upinzani  kuona chipukizi na  vijana  wa CCM wanavaa  nguo  za  kijana  wao  wakawabatiza  jina  kuwa ni Green Guard na  kuwa katika katiba ya  vijana  wa  CCM hakuna sehemu  ambayo inatamka ulinzi huo wa Green Gurd zaidi ya  wapinzani  kuwapachika majina vijana  wa CCM kwa  kuwa wanavaa nguo  za  kijani .

Hata   Hivyo Mapunda  alisema hawanampango  wowote wa  kuwafuta  vijana  hao kwani  ni  sehemu ya  jumuiya  ya  CCM kama  ilivyojumuiya  ya wazazi , UWT na Vijana  na kuwa kazi ya  jumuiya ya  vijana  wa CCM ni kushiriki kukijenga  chama  kwa  kushiriki shughuli za maendeleo na  sio  kuwaandaa kwa  kuvuruga amani kama  wapinzani  wanavyoweka makambi  vichakani  kwa ajili ya kuvuruga amani  yetu .


" Tumeendelea  kuwaona  wenzetu  wakiwaandaa  vijana wao  kwa ajili ya  kufanya  vurugu na hata  juzi Mbeya  vijana  wao  wawili  ambao  walikutwa na barua  za  viongozi wa Chadema taifa  walikamatwa na polisi wakiwa na vifaa vya  kininja jambo ambalo ni  kinyume na mafunzo ya  vijana wa CCM ambao wanapokwenda katika mafunzo wanapewa elimu ya ujasiliamali ,kushiriki kufyatua  tofari na  kazi nyingine na sio  kuwafundisha  utukutu "


Umoja  wa  vijana  wa CCM umekuwa  mbele  kuwaandaa  watoto kupitia mafunzo ya  chipukizi kwa  kuimba nyimbo  za chama na  Taifa  pamoja na  kuwafundisha namna ya  kuwaheshimu viongozi na  kuwaandaa kuwa  viongozi  bora  na  wazalendo mbeleni na  sio kuwafunza mafunzo  ya kiuharifu .

IGP Mangu  anapaswa  kutathimini  kauli  yake  na  kwanza  badala  ya  kutoa kauli  bila  kujua kwani alipaswa  kusoma katiba ya  CCM  kama  kuna  sehemu  inawataja  hao Green Guard zaidi ya  Chipukizi na  vijana .

Alisema  chipukizi  wa CCM wanaandaliwa  kwa  ukakamavu wa  kizalendo kwa  kujua  gwaride na  kuimba  nyimbo za  chama na  kitaifa  kama  ambavyo siku zote katika maadhimisho ya kitaifa kama Mwenge , uhuru na mengine ambavyo  chipukizi hao huandaliwa kwa michezo  mbali mbali.

Kwani  alisema  kuwa  nchi  hii awali  ilikuwa na  vijana  wanaojituma kufanya kazi  za  kujitegemea  na  kuwa na uchumi mzuri  ila  sasa  vijana  wamekuwa ni  wa  kushiriki maandamano ya kichochezi yanayofanywa na vyama  vya vinavyounda katiba ya  wananchi (UKAWA) na  kuwa hivi  sasa upinzani  umechangia  kukuza uvivu kwa vijana tofauti na  CCM imewafundisha  vijana  kuwa  wazalendo na  kupenda kazi.

Akithibitisha  hilo alisema kwa mkoa wa Iringa vijana  wameshiriki makambi mbali mbali ya  kufanya kazi za kimaendeleo na sasa ameagiza  vijana  wa  mkoa  wa Iringa kuweka kambi ya  kufyatua  tofari  katika  shule ya  sekondari Idodi na kuanza  ujenzi wa bweni  lililoungua moto zaidi ya mara  mbili  shuleni hapo.

Kuhusu  viongozi wa  dini  wanaotoa matamko mbali mbali  ya  kisiasa  katibu  huyo alisema  kuwa  viongozi hao  hawawatendei haki  waumini  wao na kuwa ni hatari kwa dini yoyote  nchini  kujiingiza katika  siasa kwani ni mwanzo  na mwisho wa  dini  hiyo kuyumba kwa  kukimbiwa na waumini  kutokana na ndani ya nyumba ya  ibada  kuwa na  waumini wenye  vyama tofauti .

Hivyo  alishauri  viongozi wa  dini  kuepuka kuingiza siasa ndani ya  nyumba  za ibada na badala  yake  kufanya kazi ya dini  bila kuingiza  ushabiki wa  kisiasa .

IGP Mangu hivi karibuni alivitaka  vyama vya  CCM , CUF na Chadema  kuhakikisha vinafuata muongozo uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo na kama vikienda kinyume jeshi litapambana navyo.


Alisema wamejadiliana na vyama hivyo na kwamba ofisi ya msajili imetoa muongozo ambao wanatakiwa kufuata katika kutekeleza ili waweze kufanya kazi zao kwa utaratibu unaotakiwa.

IGP Mangu alisema Katiba na sheria za nchi haziruhusu vikundi hivyo kuwepo, kwani jukumu la kulinda raia na mali zao ni la Jeshi la Polisi, hivyo vinaingilia kazi ya jeshi hilo.

“Katika mkutano huu tumekubaliana kuwa vyama vinatakiwa kufuata muongozo kutoka Ofisi ya Msajili na kama watashindwa kufanya hivyo basi sisi jeshi tuko tayari kupambana nao,”alisema IGP Mangu.

Mangu alisema mkutano huo utawasaidia kupata uelewa pole pole lakini kinachotakiwa hadi kufikia wakati wa uchaguzi mkuu vikundi vyote visiwepo.

Alisema suala la chama kuwa vikundi vya vijana vyenye misingi ambayo haivunji Katiba ya nchi ni sahihi lakini kinyume cha hapo hawezi kuvumilia hali hiyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray alisema kuna vyama ambavyo vimekuwa na vikundi vya ulinzi na kuvitaja kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

Mziray alisema historia inaonesha kuwa vikundi hivyo vilikuwa wakati wa chama kimoja hivyo kinachoonekana sasa ni vikundi hivyo kufanya kazi ya Polisi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu, sheria za nchi na katiba.

Alisema uwepo wa vikundi hivyo ni kinyume cha sheria hivyo katika mkutano huo wanajaribu kuviangalia kama undeshwaji wa vikundi hivyo kama ni sahihi au si sahihi.

“Unajua vikundi hivi vipo miaka mingi tatizo ni wakati huu vinaonekana kuwa na mitizamo tofauti jambo ambalo linahatarisha usalama wa nchi,” alisema Mziray.

Mziray alisema vyama vya siasa vinatakiwa kufuata mapendekezo yaliyotolewa kama wakishindwa jeshi litashughulika nalo.

Mbali na hayo, alisema katika mkutano huo vyama viwili ambavyo ni Chadema na CUF havikuhudhuria lakini ujumbe utawafikia na watatakiwa kutekeleza.

Aidha, Mziray alilitaka Jeshi la Polisi kusimamia misingi ya sheria katika utekelezaji wa majukumu yake kwani kinyume cha hapo ndipo migogoro inabuka kila kukicha.

Mziray alisema kitendo cha katiba za vyama vyao kubainisha vikundi hivyo na msajili kuvikubalia isiwe ni sababu ya kuruhusu migongano hiyo. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ally Vuai alisema wao hawana vikundi vya ulinzi ndani ya chama.

Alisema kuwa vijana wao hawawaandai kijeshi ila kuwa vijana bora kiitikadi na kuwa na mwamko wa kujua siasa.

“Sisi hatuwafundishi kuwa magaidi ila tunawafundisha kuwa vijana bora ila kuna muonekano wa mavazi ambao jeshi wakiona wanaweza kutia shaka, lakini kama tatizo ndiyo hilo tunaweza kurekebisha,” alisema Vuai.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwataka viongozi wa vyama kusoma sheria za nchi na kuzielewa ili wasizivunje kwa kisingizio cha kujilinda.

Mutungi alisema ofisi yake itahakikisha inawapatia elimu viongozi wa vyama ili kuhakikisha wanatambua mipaka yao ya kisheria katika kuunda vikundi hivyo.

Msajili huyo alisema ni jukumu la vyama na Jeshi la Polisi kujipanga na kukaa pamoja ili waweze kufikia muafaka kuhusu changamoto ambazo zinawakuta na si kuingia kwenye migongano.

“Unajua kinachotokea hapa ni kukosekana kwa uaminifu katika pande hizi mbili lakini wakati wa kutambua kuwa katiba na sheria za nchi zinataka nini ni huu ili kuepuka migogoro,” alisema.
CUF yanena

Naibu Mkurugenzi Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema hawawezi kufuta kikundi chao cha ulinzi (Blue Brigade) kwani kinatumika kulinda ulinzi wa mali za chama na viongozi wake.

“Polisi wenyewe wanalalamika hawatoshi kutoa ulinzi kwa wananchi wote, lakini pia sisi kama CUF hatuwezi kuacha kutoa ulinzi mathalan kwa mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Lipumba. Na hili limo kwenye katiba yetu.

“Kikundi hiki hakipo kupambana na watu, na kama kuna mahali kimefanya kosa kichukuliwe hatua…kwanza uamuzi uliofikiwa ni wa kidikteta kwani hatujashirikishwa,” alisema Kambaya.
Chadema

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kikundi chake cha ulinzi cha Red Brigade kitaendelea kuwepo hadi pale haki itakapotendeka.

Alisema lengo la kikundi chao cha ulinzi ni kulinda viongozi, mali za chama na wanachama wao katika mikutano kwani Jeshi la Polisi limeshindwa kuwajali Chadema na kuegemea upande wa CCM.

Mbowe aliongeza inaonekana hiyo ni hofu ya uchaguzi mkuu hasa kwa kuzingatia matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana, upinzani umeshinda maeneo mengi.

Alisema kuwa Jaji Mutungi ana uwezo wa kufuta vikundi hivyo kwa mamlaka aliyonayo, lakini hawezi kufuta yaliyoko moyoni kwa watu katika kujilinda.



0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa