Home » » MTAZAMO: WASOMI: JK AMEONA MBALI

MTAZAMO: WASOMI: JK AMEONA MBALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Wasomi na wachambuzi wa siasa wamesema Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameona mbali kuwataka viongozi wa chama hicho kuteua mgombea wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama wakisema bila kufanya hivyo wataangushwa na mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza jana, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema mwaka huu CCM itakuwa na ushindani mkali kuliko ilivyowahi kutokea kwenye uchaguzi wowote wa nyuma.
Alisema ushindani huo unatokana na kuwapo kwa mgombea urais wa Ukawa unaoundwa na vyama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Vyama hivyo vimeamua kushirikiana kusimamisha mgombea mmoja kwenye nafasi ya urais, ubunge na udiwani, ushirikiano huo utatoa upinzani mkali kwa CCM,” alisema Mpangala.
Alisema CCM wameliona hilo na ndiyo maana Rais Kikwete ameona ni muhimu awaeleze wana CCM kwamba wanatakiwa kuchagua viongozi wanaokubalika na wananchi walio wengi, vinginevyo watashindwa.
“Yale mambo ya zamani ya kila kundi kuwa na mgombea wake yakirudiwa hivi sasa yatakigharimu chama hicho, wanatakiwa kuungana na kuweka mtu anayekubalika bila kujali makundi,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo pia alisema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa na tofauti kubwa na chaguzi zilizopita, hivyo lazima wapate mgombea maarufu.
Akitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 alisema: “Katika kipindi hicho Mkapa (Benjamin) hakuwa akifahamika sana ukilinganisha na wana-CCM wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo lakini alishinda na kuwa rais. Mwaka huu wakijaribu kufanya hivyo wataanguka vibaya, hali ya kisiasa imebadilika,” alisema.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, viashiria vinaonyesha kuwa vyama vya upinzani vinazidi kuwa na nguvu mwaka hadi mwaka, akitaja Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita kama mfano... “Hata mgombea wa urais wa CCM, 2010 alipata kura chache ikilinganishwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Hii ina maana vyama vya upinzani vinakua kwa kasi,” alisema.
Alisema kukithiri kwa rushwa na umaskini katika jamii kumewakatisha tamaa wananchi hivyo watahitaji kiongozi mwenye uwezo kupunguza matatizo hayo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema Rais Kikwete anafahamu kuwa chama hicho kisipoweka wagombea wanaokubalika kitaanguka kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Kikwete ameliona hilo na wanachama wenzake wafahamu kuwa huu si wakati wa kuweka mtu wao, bali mtu anayekubalika na wananchi walio wengi,” alisema.
Alisema ukiacha kwenye nafasi ya urais, CCM wana mifano mingi ambayo waliweka watu wao lakini wananchi walipiga kura za hasira kuvichagua vyama vya upinzani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kauli ya Rais Kikwete imelenga kukinusuru chama hicho kutokana na nguvu kubwa ya vyama vya upinzani.
Alisema CCM ina wanachama wengi wanaokubalika ndani na nje ya chama hicho ambao mmoja wao akichaguliwa kugombea urais anaweza kukisaidia.
“Hotuba ya Kikwete inawakumbusha wanachama kuchagua watu wanaokubalika kwa sababu wapo, suala hapa anawakumbusha kuchagua mtu sahihi,” alisema.
Kuepuka makundi
Katika hatua nyingine, Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru (pichani) amesema haiwezekani kuepuka makundi ya urais katika kipindi cha uchaguzi ndani ya CCM, lakini mwisho wa siku, chama hicho kitamteua mtu anayekubalika ndani na nje ya chama.
“Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi wa kidemokrasia bila ya kuwa na makundi,” alisema Kingunge wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Uzalendo kilichorushwa na Kituo cha ITV juzi.
“Mwaka 1995 kila mgombea alikuwa na kundi lake na mwaka 2005 tulikuwa na makundi hata mwaka huu yapo,” alisema.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa