Basi la Majinja Express likiwa limeharibika vibaya baada ya kuangukiwa
na kontena katika ajali iliyotokea nje kidogo ya mji wa Mafinga jana
eneo la Changalawe barabara kuu ya Iringa Mbeya.
Msululu wa magari ukiwa unasubiri kuondolewa kwa maiti katika eneo la ajali (Picha zote na Denis Mlowe).
NA DENIS MLOWE, MUFINDI
HUZUNI na majonzi yametawala katika mji mdogo wa
Mafinga baada ya ajali mbaya ya basi la abiria la Majinja Express lilokuwa
likitokea jijini Mbeya kuelekea Dar Es salaam kugongana uso kwa uso na kisha
kudondokewa na Kontena na kusababisha watu 42 kufariki dunia katika ajali iliyotokea
eneo la Changarawe barabara kuu ya Iringa kwenda Mbeya.
Ajali hiyo ambayo hatazamiki mara mbili imetokea
majira ya 3.30 asubuhi km 5 kutoka mjini Mafinga kwa lori lenye namba T689 APJ
likiendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina la Maka Sebastian (26)mali ya CIPEX Company kwa kontena kuangukia basi la
Majinja Express lenye namba T438 CDE likiendesha na dereva Baraka Gabriel (37).
Katika
ajali hiyo waliofariki dunia papo hapo walikuwa 37 na watano wamefariki wakiwa
hospitali ya wilaya ya Mufindi na inasemekana wengi wao ni wanafunzi wa chuo
kikuu cha Dar es salaam waliokuwa wakitokea jijini Mbeya kati ya hao walofariki
ni wanaume 32 wanawake 7, watoto 3 na majeruhi 22.
Mmoja wa abiria wa basi hilo,Musa Mwasege akisimulia
chanzo cha ajali hiyo alisema kuwa chanzo ajali hiyo ni uzembe wa dereva
wa basi alilopanda kwa kuwa katika
mwendo kasi licha ya ubovu wa barabara hiyo kuwa na mashimo mengi
yanayosababisha ajali.
“Sehemu iliyotokea ajali kwa kweli ni mbovu hivyo
dereva wetu baada ya kupunguza mwendo akawa anazidi kuongeza na kutumbukia
katika shimo na kusababisha kugonga uso kwa uso na roli hilo na kisha kontena
kutuangukia baada ya hapo sikutambua lolote hadi nilipofika hospitali” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza
akizungumza katika eneo la ajali alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni ubovu
uliokithiri wa barabara hiyo na ni tukio la kuhuzunisha sana kwa wa watanzania
na kuagiza wakala wa barabara kuanza matengenezo ya barabara hiyo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani
Mungi, amekiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa chanzo cha ajali ni ubovu
wa barabara kutokana kuwa na mashimo mengi.
“Hapa tusitafute mchawi nani katika hii ajali chanzo
kikubwa ni ubovu wa barabara hivyo ni jukumu la mamlaka husika kurekebisha
tatizo la barabara.” Alisema.
Kamanda Mungi aliwataja abiria waliokuwemo katika
basi hilo kuwa ni Esta Emanuel Lusekelo, Jerimiah Wakison, Doto Katuga, Diga Solomon,
Theresia Kaminyage, Frank Chiwango, Luteni Sanga, Alfred Sanga, Juliana Bukuku,
Esta Fide, Paulina Justin.
Wengine ni Catherine Mwajengi, Zira Kasambala, Rebeka
Kasambala, Mbamba Ipyana, Dulile Kambala, Frank Mbaule, Mustapha Ramadhan,
Bwana Mussa, Shadrak Msigwa, Mathias Justin, na aliyejulikana kwa jina moja la
Elias.
Naye mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya
Mufindi Boaz Mnenegwa alikiri kupokea maiti 37 na majeruhi 22 zilizotokana na
ajali hiyo na kusema kuwa majeruhi watano walifariki mara baada kufikishwa
kituoni hapo.
Alisema kuwa kutokana ufinyu wa nafasi katika chumba
cha kulaza maiti hospitalini hapo maiti 32 zilisafirishwa kuelekea katika
hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na majeruhi waliokuwa mahututi wawili wote
wa kiume walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Chanzo: Jiachie Blog
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment