HALMASHAURI ya Wilaya ya
Kilolo imetoa msaada wa Mbuzi 18 kwa waathirika wa ugonjwa wa ukimwi wa kikundi
cha Matumaini kilichopo kijiji cha Kitumbuka, msaada wenye lengo la kuwaongezea
mtaji katika kukuza uchumi wao na kuwaepusha na hali duni.
Akikabidhi Mbuzi hao wenye thamani zaidi ya
shilingi Milioni 1 na nusu, katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani,
iliyofanyika katika Kijiji cha Kitumbuka, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Kilolo Bw. Joseph Muhumba amesema msaada huo utawawezesha waathirika hao
kuendelea kuzihudumia familia zao.
Aidha Muumba amesema jamii inatapaswa kufahamu
kuwa waathirika wa ugonjwa wa ukimwi wanauwezo wa kuchangia shughuli za
maendeleo kwa kufanya kazi, huku akiwataka wananchi kutambua kuwa kupata
maambukizi sio mwisho wa maisha.
Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano, cha
wanaoishi na Virusi vya ukimwi Bw. Leonard Chusi amesema msaada huo unaongeza
imani kwao ya kuwa jamii inawajali, tofauti na awali jamii ilivyokuwa na tabia
ya kunyanyapaa, jambo lililochangia baadhi yao kupoteza maisha kwa hofu.
Naye mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Wilaya ya
Kilolo Faraja Chaula amesema Wilaya hiyo ina asilimia 9.1 cha watu wanaoishi na
Virus vya Ukimwi, na kuwa sababu kubwa ya tatizo hilo ni pamoja na jamii
kuendekeza mila na destuli potofu zilizopitwa na wakati.
Bi. Chaula amesema pia tatizo la ulevi wa
kupindukia na jamii kutotumia Kondomu kwa usahihi wakati wa kujamiiana ni
sababu zinazochangia maambukizi mpya ya VVU na hivyo kuwepo na idadi kubwa ya
waathirika wa ugonjwa huo wa Ukimwi.
0 comments:
Post a Comment